Home | Terms & Conditions | Help

November 24, 2024, 6:11 pm

SPORT: ZIFAHAMU SABABU KUU 6 ZILIZOPELEKEA YANGA KUCHUKUA UBINGWA VPL

DAR ES SALAAM: Hatimaye lingi ya Tanzania bara maarufu kwa jina la VPL imemalizika kwa Yanga kubeba ubingwa wa 2016/2017 si kwa kubahatisha bali ni kwa mipango na kujituma kwa wachezaji tofauti na watu wanavyodhani kwamba mabingwa hao wamebeba ndoo kwa bahati mbaya.

Uongozi wa Simba ulijipanga kuhakikisha msimu huu ubingwa unabaki Msimbazi, walifanya maandalizi mazuri na mapema kwa kuweka kambi mkoani Morogoro na wakafanikiwa kufanya vizuri katika mechi za raundi ya kwanza.

Yanga wamewapiku Simba uwanjani na nje ya uwanja. Kikosi cha Yanga kilikuwa na wachezaji wengi wazoefu na walioipa ubingwa timu hiyo katika msimu uliopita ukiacha wachache walioongozwa badae wakati Simba ilitawaliwa na wachezaji wengi wageni katika kikosi chao.

Tuangalie mambo kadhaa ambayo yaliipa Yanga ubingwa wa VPL ukilinganisha na Simba katika msimu uliomalizika Mei 20, 2017.

1. Uongozi

Uongozi wa Yanga ulikuwa haujatulia kama wa Simba. Kuna baadhi ya viongozi waliondoshwa kwenye kamati ya utendaji ya Yanga kwa mfano Salum Mkemi na Hashimu Abdallah. Hata hivyo badae waliacha malumbano kwenye vyombo vya habari na kuamua kuwa kitu kimoja, baadhi ya wanachama wakarudishwa kwenye timu na wengine kurudishwa kwenye uongozi utulivu ukapatikana

2. Mashabiki wa Yanga

Mara zote mashabiki wa Yanga wamekuwa na umoja bila kujali timu yao inapita katika wakati gani. Iwe ni kipindi cha changamoto au amani ndani ya klabu siku zote mashabiki wa Yanga huzungumza lugha moja badala ya kugawanyika katika makundi kama ilivyo kwa wenzao wa Simba.

3. Wadau

Waliungana mapema baada ya uongozi kutetereka na kutafuta njia mbadala ya kuhakikisha wanawapoza wachezaji wa Yanga licha wachezaji kudai mishahara kwa miezi kadhaa. Waliwatengenezea mfumo mzuri wa bonus na posho ili hata kama wakikosa mishahara yao, posho iwasaidie kukabili makali ya maisha.

4. Vikosi

Watu wengi walitegemea Yanga wangeharibu mechi zao katika kipindi cha mwisho cha msimu kulingana na matatizo yaliyokuwa yanaiandama klabu yao, lakini ndio kipindi ambacho wachezaji waliungana na kuhakikisha wanashinda kila mechi licha ya mechi nyingi kuwa ngumu. Walikuwa wanashinda katika mazingira magumu licha ya wakati mwingine kuzidiwa katika mchezo lakini wao kikibwa ilikuwa ni pointi tatu.

Kikosi cha Yanga kina wachezaji wanaoweza kukuamua matokeo ya mechi kwa mchezaji mmojammoja, mchezaji kama Amis Tambwe, njaa binafsi aliyokuwanayo mtu kama Msuva pamoja na matatizo ya kutolipwa mshahara kwa miezi mitatu lakini alikuwa na kitu binafsi alichotaka kuonesha.

Obrey Chirwa ni mchezaji ambaye aliiweka Yanga mabegani katika raundi ya pili, angalia upambanaji wa Thabani Kamusoka, Haura Niyonzima alivyokuwa anajitoa, kuna wakati Vicent Bossou aligoma kutokana na kuto lipwa mishahara lakini unatakiwa kujiuliza kwa nini alirejea na akawa mhamasishaji? Hapo utagundua uongozi na wadau walitafuta njia mbadala ya kurudisha morali ya wachezaji .

5. Ushindani wa nafasi kwenye kikosi cha kwanza

Juma Abdul vs Hassani Kessy kila aliyepata nafasi alijitahidi kuonesha kwamba anastahili kuanza kwenye kikosi cha kwanza, magolikipa Ally Mustafa ‘Barthez’, Deogratius Munishi na Beno Kkolanya wote kwa pamoja walipeana changamoto na kila aliyepata nafasi alitaka kuonesha utofauti na yule aliyepo kwenye benchi.

Ushindani kati ya Vicent Andrew ‘Dante’, Kelvin Yondani, Nadir Haroub Cannavaro na Vicent Bossou, katika hali ya kawaida watu walitarajia kungekuwa na wachezaji wawili au watatu ambao wangekuwa wanaanza katika kila mechi lakini wote wanne walicheza nah ii ni kutokana na kila aliyepata nafasi kutaka kuthibitisha anastahili kucheza.

Wachezaji wa Simba walikuwa wanacheza lakini ukiangalia vizuri huoni kama wana njaa ya kutafuta kitu kwa kujitoa ukilinganisha na wachezaji wa Yanga.


6. Ratiba

Raundi ya kwanza Simba walicheza mechi nyingi nyumbani wakafanya vizuri wakati huo Yanga walikuwa wanatoka sana kwenda mikoani, raundi ya pili ikawa ni kinyume. Yanga walivyoanza kuutumia uwanja wa taifa katika raundi ya pili hawakuacha pointi na wakati huo walifanya vizuri katika mechi za ugenini za raundi ya kwanza.

Simba hawakufanya vizuri katika mechi zao za ugenini kwenye raundi ya pili hususan mechi za Kanda ya Ziwa ambako ndipo walipouacha ubingwa baada ya kuambulia pointi nne kati ya tisa


#shaffihdauda