Home | Terms & Conditions | Help

November 25, 2024, 7:23 pm

SPORT NEWS: ULIMWENGU AFANYIWA UPASUAJI WA GOTI AFRIKA KUSINI

AFRIKA KUSINI: MSHAMBULIAJI wa kimataifa wa Tanzania, Thomas Emmanuel Ulimwengu atarudi nje ya Uwanja kwa miezi sita kufuatia kufanyiwa upasuaji wa goti mjini Cape Town nchini Afrika Kusini jana mchana.


Mchezaji huyo wa AFC Eskilstuna ya Ligi Kuu ya Sweden, Ulimwengu amesema kwamba amefanyiwa upasuaji huo katika hospitali ya Taasisi ya Sayansi ya Michezo Afrika Kusini na ameambiwa atakaa nje hadi Januari.

Ulimwengu amesema kwamba baada ya kufanyiwa upasuaji huo ataendelea kuwa nchini humo kwa wiki mbili zaidi.


“Ninabaki hapa, kwani tayari nimeanza programu maalum ya mazoezi ninayofanyishwa na Daktari hapa hapa,”amesema Ulimwengu.

Maumivu ya goti yamekuwa yakimsakama Ulimwengu tangu alipojiunga na Eskilstuna Januari mwaka huu akitokea Tout Puissant Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) kiasi cha kushindwa kucheza.

Ulimwengu aliyezaliwa Juni 14, mwaka 1993 aliibukia katika taasisi ya soka Tanzania (TSA) mwaka 2008, kabla ya mwaka 2009 kwenda kuanza kukomazwa Ligi Kuu katika klabu ya Moro United alikokuwa akicheza kwa mkopo hadi mwaka 2010 alipokwenda akademi ya AFC Eskilstuna ya Sweden, alikocheza hadi mwaka 2011 alipochukuliwa na timu ya vijana ya Mazembe.

Alicheza U-20 ya Mazembe kwa msimu moja kabla ya kupandishwa rasmi timu ya wakubwa mwaka 2012 na moja kwa moja kuwa mchezaji wa kikosi cha kwanza hadi anamaliza Mkataba wake Oktoba mwaka jana.

Ulimwengu amehamia Ulaya baada ya kushinda mataji makubwa akiwa na Mazembe kama Ligi ya Mabingwa Afrika, Super Cup ya Afrika na pamoja na kucheza Klabu Bingwa ya Dunia.