Home | Terms & Conditions | Help

November 26, 2024, 2:31 am

SPORT NEWS: SIRI ZITO YAIBUKA UCHAGUZI TFF

DODOMA: IKIWA ni siku nne tu zimepita tangu Shirikisho la soka Tanzania (TFF) kufanya uchaguzi na kuwapata viongozi wake, baadhi ya waliokuwa wagombea katika uchaguzi huo wameibuka na kutoa yaliyo moyoni mwao.


Katika uchaguzi huo uliofanyika kwenye ukumbi wa St Gasper uliopo mkoani Dodoma, Wallace Karia alichaguliwa kuwa Rais mpya wa TFF huku Michael Wambura akichaguliwa kuwa Makamu wa Rais.

Katika taarifa yake kwa vyombo vya habari, aliyekuwa mgombea wa urais, Shija Richard, pamoja na kuwapongeza washindi katika uchaguzi huo, alisema mchakato mzima uligubikwa na ‘usiri’ na kuwafanya baadhi ya wagombea kutokuwa na imani na kile kilichokuwa kikiendelea katika mchakato mzima wa upigaji na kuhesabu kura.

“Niombe uongozi mpya ulioingia madarakani kubadilisha kasoro za kikatiba zinazoweza kutia mashaka mchakato mzima wa uchaguzi, kwa mfano Kamati ya Uchaguzi kuteuliwa na wajumbe wa Kamati ya Utendaji ambao ni wagombea hii ni kasoro kubwa inayoweza kutia mashaka uhuru wa Kamati hiyo,” alisema Shija..

Alisema kuna haja ya kubadilisha katiba ili inapotokea mchakato wa uchaguzi umeshaanza na kunahitajika mabadiliko ya Kamati ya Uchaguzi, taasisi nyingine huru ipewe jukumu la kubadilisha Kamati ya Uchaguzi.

“Rais na Kamati yake ya Utendaji wawe na uwezo wa kuteua Kamati ya Uchaguzi pale tu mchakato wa uchaguzi unapokuwa haujaanza, lakini ukianza alafu rais ambaye pia ni mgombea anapoteua kamati ya uchaguzi inatia wasiwasi,” alisema Shija.

Malalamiko kama hayo pia yalitolewa na Fredrick Mwakalebela aliyekuwa mgombea wa nafasi ya Urais katika uchaguzi huo.

Mwakalebela ambaye ni Katibu Mkuu wa zamani wa TFF, alisema kuwa kitendo cha mgombea mmoja ambaye alikuwa ndani ya uongozi uliomaliza muda wake kutoulizwa swali wakati wa kujinadi kwa wajumbe kunatia shaka.

“Ni kitu ambacho akiingii akilini, mgombea mmoja kutoulizwa swali wakati alikuwepo kwenye uongozi ambao unatuhumiwa kwa ubadhilifu, na hata kitendo cha kutoruhusiwa kulinda kura zetu na kuwaondoa wajumbe nje mara baada ya kupiga kura kinatia shaka, tutaamini vipi kama haki ilitendeka,” alisema Mwakalebela.

Hata hivyo wagombea hao waliwatakia heri viongozi wote walichaguliwa katika kutimiza majukumu yao wakiwa viongozi wapya wa TFF.