Home | Terms & Conditions | Help

November 26, 2024, 2:33 am

SPORT NEWS: SIMBA YAGOMA KUMUUZA KICHUYA KWA WAARABU

DAR ES SALAAM: UONGOZI wa mabingwa wa Kombe la FA, Simba wamekataa kumuuza mshambuliaji wao Shiza Kichuya imefahamika.

Kichuya alikuwa anatakiwa na klabu moja inayoshiriki Ligi Kuu ya Soka Misri ambayo ilikuwa tayari kumnunua kwa dau la Dola za Marekani 80,000 (zaidi ya Sh. Milioni 165 za Tanzania).


Taarifa zilizopatikana kutoka kwa viongozi wa Simba zinasema kuwa wamefikia uamuzi wa kukataa kumuuza nyota huyo kwa malengo ya kuona klabu yao inafanya vizuri katika msimu ujao wa Ligi Kuu Tanzania Bara na mashindano ya Kombe la Shirikisho Afrika watakayoshiriki.


"Tumefanya vikao zaidi ya viwili kuhusiana na mshambuliaji huyo, lakini uamuzi wa mwisho ni kuwa hauzwi," alisema kiongozi mmoja wa juu wa Simba.

Chanzo chetu kinasema kuwa kabla ya viongozi wa Simba kufikia uamuzi wa kumuuza Kichuya, walihitaji kumwangalia mshambuliaji wao mpya kutoka Ghana, Nicholas Gyan kama ataweza kuziba pengo lake na jibu tulilopata ni mpaka awazoee wenzake, hatumuuzi tena," alisema kiongozi huyo.


Kichuya ambaye ni mchezaji wa timu ya Taifa (Taifa Stars) alijiunga na Simba msimu uliopita akitokea Mtibwa Sugar ya Manungu, Turiani Morogoro na mkataba wake na Wekundu wa Msimbazi umebakiza mwaka mmoja.

Kikosi cha Simba kiko Zanzibar kikiendelea na mazoezi kwa ajili ya kujiandaa kuwakabili mahasimu wao Yanga katika mechi ya Ngao ya Jamii itakayofanyika Agosti 23 mwaka huu kwenye Uwanja wa Taifa jijini.

Tayari beki wake tegemeo Mganda Murshid Juuko amerejea nchini tayari kujiunga na wenzake kwa ajili ya kujiandaa na msimu mpya wa ligi ambao Wekundu wa Msimbazi wataanza kwa kucheza na Ruvu Shooting ya Pwani kwenye Uwanja wa Taifa.