Home | Terms & Conditions | Help

November 25, 2024, 5:27 pm

SPORT NEWS: MSUVA APEWA BARAKA ZOTE NA WAZEE WA YANGA

DAR ES SALAAM: Wazee wa Yanga wamesema wanamtakia mafanikio mema kiungo mshambuliaji wake, Simon Msuva anayetarajia kujiunga na Klabu ya Difaa El Jadidi inayoshiriki Ligi Kuu ya Morocco.
Katibu wa Baraza la Wazee la Yanga, Ibrahim Akilimali amesema kuwa kwa upande wao wanatoa baraka zote kwa mchezaji huyo ili aweze kufanikiwa zaidi baada ya kuitumikia Yanga kwa mafanikio makubwa.


“Leo (jana) tulikuwa na kikao cha Baraza la Wazee wa Yanga na kikubwa ilikuwa ni kujadili suala la kijana wetu Msuva ambaye ameuzwa kwenda kucheza soka Morocco, wazee wa Yanga kwa upande wetu tumeridhia kuondoka kwake.

“Unajua kwa upande wetu ni heshima kubwa kwa klabu yetu kufungua milango ili vijana wetu waweze kucheza soka la kulipwa, mafanikio aliyotuachia ni makubwa na tunayaheshimu kwa sababu siku akiamua kurejea kucheza hapa atarudi kwenye timu yake ambayo imemkuza na kumpa mafanikio,” alisema Akilimali.



Klabu hiyo ya Morocco iliyoshika nafasi ya pili msimu uliopita, imekubali kumlipa Msuva mshahara wa dola 4,000 (Sh 9m), kiasi ambacho awali aligoma akidai ni kidogo kwa sababu anakwenda kuishi ugenini.

Wakati huohuo, Msuva amesema anajua mazingira anayoenda kukutana nayo huku akipanga kuonyesha uwezo wa juu ili kuingia kwenye kikosi cha kwanza.

“Kabla ya kukubali dili la kutimkia Difaa El Jadidi, nilipata muda wa kuitazama ligi yao kubaini aina gani ya mbinu wanazitumia na nimegundua ni kama hapa Tanzania tu yaani hakuna tofauti yoyote ile.


“Kule wanatumia mawinga zaidi kwenye kutengeneza mabao kwa kupiga mipira mirefu pamoja na pasi za haraka, sasa ukiangalia mbinu hiyo mimi nimeicheza sana Yanga na ndiye nilikuwa injini ya kutengeneza mabao, jambo hilo linanipa matumaini ya kuona kwamba sitapata shida ya kufiti na kuingia kwenye mfumo wao,” alisema Msuva.