Home | Terms & Conditions | Help

November 26, 2024, 7:32 pm

SPORT NEWS: FDL YAENDELEA KUTIMU VUMBI MKOANI DODOMA.

DODOMA: Ligi daraja la kwanza FDL msimu wa 2017/18 imeendelea kutimua vumbi ambapo katika Dimba la Jamhuri mjini Dodoma,Timu ya soka ya Dodoma imeibuka na ushindi wa bao moja bila dhidi ya kikosi cha Pamba TP Lindanda ya mkoani Mwanza.

Timu ya soka ya Dodoma iliyo chini ya kocha Jamhuri Kiwelo Julio imeanza vyema mchezo wake huo wa kwanza kwa ajili ya kusaka tiketi ya kushiriki Ligi kuu soka Tanzania bara ambapo wadau pamoja na mashabiki wa soka wamekuwa na uchu wa kushuhudia timu hiyo ikicheza ligi kuu ya Tanzania Bara msimu ujao

Akizungumza mara baada ya kukamilika kwa mtange huo ambapo goli la Dodoma Fc lilifungwa na James Mendi kwa mkwaju wa Penati katika Dakika ya 83,Kocha wa Dodoma Fc Jamhuri Kiwelo Julio ameomba ushirikiano wa wadau ili kuhakikisha timu hiyo inapaa ligi kuu huku akikiri kuwa bado kuna ushindani mkubwa.

Kwa upande wake msemaji wa Pamba TP Lindanda Johnson James alisema wamejipanga kuhakikisha wanafanya vizuri katika mechi zijazo huku akimlaumu muamuzi wa mchezo kwa madai kuwa amefanya maamuzi ya upendeleo kwa kuipa ushindi Dodoma FC

Baadhi ya wadau wa soka mkoani Dodoma akiwemo mbunge wa jimbo la Dodoma Antony Mavunde walisema kuwa Dodoma ni makao makuu hivyo kuna kila sababu ya wakazi wa Dodoma kuiunga mkono timu hiyo ili iweze kufanya vizuri na hatimaye kucheza ligi kuu soka Tanzania Bara.

Ligi Daraja la Kwanza (FDL) kwa msimu wa 2017/18 inachezwa katika makundi matatu ya timu nane nane kwa mtindo wa nyumbani na ugeni.