- BREAKING NEWS: TANZANIA YAKANUSHA KUWASHIKILIA KINA DR SLAA NA MWAMBUKUZI
- BREAKING NEWS: RAIS WA MAPINDUZI WA NIGER AMTEUA WAZIRI MKUU MPYA
- BREAKING NEWS: SHILINGI YA KENYA YAPOROMOKA VIBAYA DHIDI YA DOLA
- BREAKING SEREKALI YA RWANDA YAKASIRISHWA NA UBELGIJI KUTOMUIDHINISHA BALOZI WAKE
- BREAKING NEWS: RAIS KIM AKUTANA NA WAZIRI WA ULINZI WA URUSI
SPORT: MWINYI ZAHERA AFUNGIWA VIRAGO YANGA
HATIMAYE klabu ya Yanga SC imeachana na kocha wake, Mwinyi Zahera raia wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) baada ya kipindi cha miezi 15 na ushei tangu apewe nafasi hiyo.
Uamuzi huo umetangazwa leo na Mwenyekiti wa Yanga SC, Dk. Mshindo Msolla katika mkutano wake na Waandishi wa Habari mchana wa leo makao makuu ya klabu, Jangwani mjini Dar es Salaam na sasa kiungo na Nahodha wa zamani wa klabu hiyo, Charles Boniface Mkwasa ‘Master’ atakuwa kocha wa muda.
“Tumefikia maamuzi kama Kamati ya Utendaji ya kuachana na benchi lote la ufundi la klabu ya Yanga. Maana yake ni nini, ni kwamba tumeachana salama na mwalimu Kocha Mkuu Zahera, salama na kocha Noel Mwandila na tutaachana salama na benchi lote la ufundi kaunzia Meneja mpaka mlinzi,”amesema Dk Msolla.
Aidha, Mwenyekiti huyo wa Yanga amesema kwamba wamekubaliana katika kikao cha Kamati ya Utendaji kuanza upya na wafanyakazi wote wa benchi la Ufundi wameondolewa.
“Maana yake ni kwamba tumeamua tuanze upya, kama mtu atarudi, atarudi kwa utaratibu mwingine, lakini kwa leo na maamuzi ya Kamati ni kwamba tuanze upya. Sasa tulikuwa na kikao kwanza na walimu ndiyo maana tumechelewa tulikuwa na walimu wote wawili, tuongea kila kitu, tumepitia mikataba, tumeridhiana na tunaendela na taratibu nyingine za kuachana salama,”amesema.
Uamuzi unakuja siku mbili baada ya Yanga SC kutolewa kwenye michuano ya Kombe la Shirikisho kufuatia kuchapwa 3-0 na wenyeji, Pyramids FC Uwanja wa Jeshi la Anga wa Juni 30 mjini Cairo katika mchezo wa marudiano wa mchujo wa kuwania kuingia hatua ya makundi, hivyo kutolewa kwa jumla ya mabao 5-1 kufuatia kufungwa 2-1 kwenye mchezo wa kwanza mjini Mwanza Jumapili wiki iliyopita.
Zahera alijiunga na Yanga SC Mei mwaka jana akichukua nafasi ya Mzambia, George Lwandamina – na baada ya kuwa timu kwa miezi 15 bila kushinda taji lolote ameondolewa kwa pamoja na benchi lake zima la Ufundi.
Aliyekuwa Msaidizi wake, Mzambia Noel Mwandila, Meneja Hafidh Saleh, Mtunza Vifaa, Mohamed Omar ‘Mpogolo’, Mchua Misuli, Jackob Onyango na Daktari Edward Bavu nao wanafuatana na bosi wao, wakati kipa wa makipa pekee Manyika Peter ndiye amependekezwa kubaki.
Katika kipindi cha miezi 15, Zahera ameiongoza Yanga katika jumla ya mechi 75 za kirafiki na mashindano, kati ya hizo akishinda 45, kufungwa 17 na sare 13.
Msimu uliopita Yanga SC ilimaliza nafasi ya pili katika Ligi Kuu, nyuma ya Simba SC waliobuka mabingwa, wakati katika Kombe la Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), maarufu kama Azam Sports Federation Cup (ASFC) ilitolewa katika Nusu Fainali na Lipuli FC ya Iringa.
Msimu huu Yanga ilianzia katika Ligi ya Mabingwa Afrika na baada ya kuitoa Township Rollers ya Botswana kwa jumla ya mabao 2-1, ikitoa sare ya 1-1 Dar es Salaam na kushinda 1-0 Gaborone, ikaenda kutolewa na Zesco United ya Zambia kwa jumla ya mabao 3-2, ikitoka sare ya 1-1 nyumbani na kwenda kufungwa 2-1 Ndola.
Ndipo ikaangukia kwenye kapu la kuwania kucheza hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika na baada ya kutolewa na Pyramids FC amepoteza ajira
Katika Ligi Kuu hadi sasa msimu huu, Yanga SC imecheza mechi nne na kushinda mbili, sare moja na kufungwa moja pia.