Home | Terms & Conditions | Help

November 24, 2024, 12:10 pm

SPORT: LWANDAMINA UBINGWA KWANZA MATATIZO KANDO

Dar es salaam: Kocha wa klabu ya Dar es salaam Young Africans, George Lwandamina amewataka vijana wake kuweka matatizo kando na kuelekeza nguvu zao katika michezo iliyosalia ya Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara na kuhakikisha wanatetea ubingwa wao Kocha George Lwandamina amesema ni lazima waweke matatizo kando kama wanataka kuutwaa ubingwa wa Ligi Kuu.

Kikosi hiko cha Dar Young Africans kimerejea jana jijini Dar es Salaam kikitokea Mkoani Geita ilipokwenda kuweka kambi fupi na kucheza mchezo mmoja wa kirafiki, ikitokea Mwanza ambako Jumapili iliyopita ilivuliwa ubingwa wa Kombe la Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), michuano inayojulikana kama Azam Sports Federation Cup (ASFC) kwa kufungwa 1-0 na wenyeji, Mbao FC katika Nusu Fainali.

“Tunahitaji kuwa kitu kimoja kwa sasa, tuweke matatizo yetu kando kwa ajili ya heshima zetu na tumalizie msimu vizuri na kwa furaha kwa kuchukua angalau ubingwa wa Ligi Kuu, ninaamini vijana wanaelewa umuhimu wa hilo,” Ni maneno ya Lwandamina.


Yanga inatarajiwa kushuka dimbani kesho katika uwanja wa Taifa, Dar es Salaam kumenyana na wajela jela, Prisons ya Mbeya katika mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara.

Mchezo huo ni miongoni mwa viporo viwili vilivyokuwa Yanga tangu mwezi uliopita. Kiporo kingine ni kile cha Toto Africans ya Mwanza.


Klabu hiyo yenye maskani yake mitaa ya jangwani inashika nafasi ya pili kwenye msimamo wa Ligi Kuu, ikiwa na alama 56 baada ya kucheza mechi 25, nyuma ya vinara, Simba SC wenye alama 59 ikishuka dimbani mara 27.
Azam FC inafuatia kwa mbali kabisa nafasi ya tatu kwa alama zake 46 za mechi 27, sawa na Matajiri wa sukari klabu ya Kagera Sugar yenye alama 46 ikishuka dimbani mara 26.


Matatizo yanayoikabili klabu hiyo mpaka inaonekana kusua sua katika mbio za Ubingwa mwaka huu ni kutokana na hali mbaya ya kifedha iliyojitokeza klabuni hapo mara baada ya mwenyekiti na mfadhili wa klabu, Yussuf Manji kuingia kwenye matatizo na Serikali mwezi Januari, mwaka huu.