Home | Terms & Conditions | Help

November 26, 2024, 3:44 pm

SPIKA: NI BORA SEREKALI INGEANZA NA BANDARI BAGAMOYO KULIKO RELI YA SGR

Spika wa Bunge la Tanzania, Job Ndugai amesema ujenzi wa bandari ya Bagamoyo mkoani Pwani ukikamilika utakuwa na tija kubwa kwa nchi, kuliko hata ujenzi wa reli ya kisasa (SGR) unaojengwa, kutoka Dar es salaam kwenda Morogoro.

“Yaani bora tungeanza na bandari hii ya kisasa kabisa tukaja reli (SGR).” Spika amesema kukamilika kwa reli ya SGR bila kuwa na bandari ya kisasa kama hiyo ambayo ilikuwa ijengwe Bagamoyo ni kazi bure kwani mpaka sasa nchini hakuna bandari nzuri hivyo Serikali inapaswa kuliona hili.

Spika Ndugai amesema hayo leo Jumatatu Mei 13, 2019 bungeni baada ya wabunge mbalimbali kuhoji mradi huo wa bandari kukwama wakati wakichangia hotuba ya bajeti ya wizara ya ujenzi, uchukuzi na mawasiliano ya mwaka 2019/20 ya Sh4.9 trilioni.

Spika Ndugai pamoja na wabunge wamemtaka Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Isack Kamwelwe pindi atakapokuwa akihitimisha mjadala wa bajeti yake leo Jioni aje na ufafanuzi wa kipi kimekwamisha ujenzi wa Bandari ya Bagamoyo mkoani Pwani kutojengwa wakati mdhabuni wa Mradi huo kupatikana na inadaiwa anatoka China. Wakati Spika akitoa maelekezo hayo, wabunge wa pande zote walikuwa wakimshangilia.

Pia Baadhi ya wabunge wengine ambao wamechangia na kuhoji bandari hiyo kutojengwa na wakihitaji ufafanuzi ni Hussein Bashe (Nzega Mjini-CCM), Lucy Magereli (Viti Maalum-Chadema), Ally Salehe (Malindi-CUF), Charles Tizeba (Buchosa-CCM) na Dk Shukuru Kawambwa (Bagamoyo-CCM)