Home | Terms & Conditions | Help

November 26, 2024, 10:42 pm

RAIS MAGUFULI: WATANZANIA WANATAKA FURAHA SIO KIFUNGWA FUNGWA

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli amekutana na kuwapongeza wachezaji wa Timu ya Taifa ya Tanzania (Taifa Stars) kwa kufanikiwa kufuzu kucheza fainali za michuano ya soka Barani Afrika kwa mwaka 2019 (AFCON-2019) na pia amempongeza bondia Hassan Mwakinyo ambaye juzi alishinda pambano lake dhidi ya bondia Sergio Gonzalez wa Argentina lililofanyika Jijini Nairobi nchini Kenya.

“Kwa kweli jana nilifurahi sana jinsi mlivyokuwa mnacheza na jinsi mlivyofunga magoli, Watanzania wanataka furaha, sio kufungwafungwa kama mlivyofungwa kule Lesotho, ile iliniuma sana hadi nilipanga kuwa sitaita tena timu kuja hapa Ikulu, lakini sasa safi."

Hafla ya kuwapongeza wanamichezo hao imefanyika leo Machi 25, 2019 Ikulu Jijini Dar es Salaam na kuhudhuriwa na Makamu wa Rais Mhe. Samia Suluhu Hassan, Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa, Viongozi wa Shirikisho la Mpira wa Miguu nchini (TFF), Kamisheni ya Ngumi Tanzania (TPBRC) na Kamati ya Ushindi ya Taifa Stars iliyoongozwa na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Mhe. Paul Makonda.

Akizungumza katika hafla hiyo Mhe. Rais Magufuli ameelezea kufurahishwa kwake na matokeo ya mchezo wa jana ambapo Taifa Stars iliifunga Timu ya Taifa ya Uganda (The Cranes) katika uwanja wa Taifa Jijini Dar es Salaam kwa magoli 3-0 na ameahidi kuwa Serikali itaendelea kuunga mkono juhudi za wanamichezo wote kwa kuwa mafanikio yao yanaliletea Taifa sifa na heshima na pia yanatangaza fursa mbalimbali ikiwemo utalii, biashara na uwekezaji.

Mhe. Rais Magufuli amewapongeza wachezaji wa Taifa Stars, viongozi wa TFF, Kamati ya Ushindi ya Taifa Stars na Watanzania wote kwa kuungana pamoja kuishangilia timu yao katika mchezo wa jana bila kujali tofauti zao za kidini, itikadi za kisiasa, makabila na kanda wanazotoka.

Nataka niwahakikishie Serikali ipo na nyinyi na ni matarajio yangu kuwa mtajiandaa vizuri ili mkafanye vizuri katika michuano ya AFCON huko Misri, sasa vita imeanza” amesema Mhe. Rais Magufuli.

Mhe. Rais Magufuli ametoa changamoto kwa wadau wote wa michezo kuhakikisha wanasimamia uboreshaji wa miundombinu ya michezo, wanajipanga vizuri kwa michezo mbalimbali ya kuiwakilisha nchi, wanarekebisha dosari zote zilizosababisha kusuasua kwa Tanzania katika michezo ya kimataifa na ameipongeza TFF kwa kufanikiwa kurejesha mgao wa fedha za maendeleo kutoka Shirikisho la Soka Duniani (FIFA).

Aidha, ameiagiza Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo kufuatilia uendeshaji wa uwanja wa Taifa ili kujiridhisha juu ya mapato na matumizi ya fedha za uwanja huo pamoja na kuangalia ubora wake kutokana na kuwepo kwa taarifa kuwa maeneo yanayoharibika hayafanyiwi matengenezo inavyopaswa.

Mhe. Rais Magufuli amempongeza bondia Hassan Mwakinyo kwa ushindi alioupata hapo juzi baada ya kumpiga kwa knockout bondia Sergio Gonzalez wa Argentina katika pambano lisilo la ubingwa lilifanyika Jijini Nairobi nchini Kenya, pamoja na mapambano mengine ambayo alishinda na amemtaka kuendelea kufanya vizuri katika mapambano mengine ili kuipatia sifa Tanzania.

“Nafahamu kuwa unazo changamoto nyingi ambazo hukusema hapa, lakini nakupongeza sana, juzi umemtandika yule jamaa mpaka akakaa chini na huwa nakuona unavyofanya mazoezi makali kwa kutumia matairi, wewe ni kijana safi sana” amesema Mhe. Rais Magufuli.

Mhe. Rais Magufuli ameipongeza kampuni ya Serengeti Breweries Limited ambayo ni wadhamini wa timu ya Taifa Stars na SportPesa ambao ni wadhamini wa bondia Hassan Mwakinyo kwa mchango wao mkubwa wa kuendeleza michezo.

Katika hafla hiyo Mhe. Rais Magufuli amekubali maombi yaliyotolewa na Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo ya kusaidiwa maandalizi ya michuano ya AFCON kwa vijana wa chini ya miaka 17 iliyopangwa kuanza tarehe 14 Aprili, 2019 hadi tarehe 28 Aprili, 2019 Jijini Dar es Salaam huku Tanzania ikiwakilishwa na timu ya Serengeti Boys, ambapo amesema Serikali itatoa shilingi Bilioni 1 kusaidia maandalizi hayo.

Halikadhalika Mhe. Rais Magufuli ametoa zawadi ya kiwanja kimoja cha kujenga nyumba Jijini Dodoma kwa kwa kila mchezaji wa Taifa Stars, Bondia Hassan Mwakinyo, mchezaji wa zamani na Nahodha wa Taifa Stars Leodgar Tenga na mchezaji wa zamani na mfungaji wa bao lililoiwezesha Tanzania kucheza robo fainali ya AFCON mwaka 1980 Peter Tino ambaye pia amezawadiwa shilingi Milioni 5.

Kwa upande wao wachezaji wa Taifa Stars ambao wameongozwa na Nahodha Msaidizi Himid Mao na bondia Hassan Mwakinyo wamemshukuru Mhe. Rais Magufuli na Serikali kwa ushirikiano mkubwa walioupata hadi kufikia mafanikio hayo na wamemuahidi kuendelea kufanya vizuri katika michezo inayofuata.

Rais wa TFF Bw. Wallace Karia na Mwenyekiti wa Baraza la Michezo la Taifa (BMT) Bw. Leodgar Tenga wamesema baada ya kufuzu kucheza fainali za AFCON sasa Taifa Stars inaelekeza nguvu zake kujiandaa na michuano hiyo mikubwa Barani Afrika na pia wameelezea matumaini makubwa ya Tanzania kufanya vizuri katika michuano ya AFCON kwa vijana wa chini ya miaka 17 ambapo Tanzania itawakilishwa na timu ya Serengeti Boys, michuano ya AFCON kwa wanawake ambapo Tanzania inawakilishwa na Twiga Stars na kufanya vizuri kwa timu ya Taifa ya Soka chini ya miaka 20 (Ngorongoro Heros) ambayo tarehe 31 Machi, 2019 itacheza na Eritrea Mjini Asmara.

Pamoja na kuwapongeza wachezaji wa Taifa Stars na Bondia Hassan Mwakinyo Mhe. Rais Magufuli amekula chakula cha mchana na wachezaji hao.