Home | Terms & Conditions | Help

November 24, 2024, 7:38 am

RAIS MAGUFULI : SEREKALI HAITAFUNGA MIPAKA WALA KUWAZUIA WATU KUTOKA NDANI

Dar es Salaam. Rais wa Tanzania, John Pombe Magufuli amesema Serikali haitafunga mipaka wala kuwazuia watu kutoka ndani ili kujikinga na maambukizi ya virusi vya corona adai kuwa kufanya hivyo kutasababisha madhara ndani na nje ya Tanzania kwa kuwa Tanzania inategemewa na nchi 8.

. Rais wa Tanzania, John Pombe Magufuli

Mapema leo Waziri wa Afya nchini Tanzania, Ummy Mwalimu alieleza hali ya ugonjwa huo akibainisha kuwa wagonjwa wamefikia 32, watano wamepona na waliofariki dunia wakifikia watatu baada ya leo kufariki wawili.

Rais Magufuli ametoa kauli hiyo leo Ijumaa Aprili 10, 2020 katika Kanisa Katoliki Parokia ya Mlimani Wilaya ya Chato mkoani Geita alipoungana na waumini kusali ibada ya Ijumaa Kuu iliyoongozwa na Padri Innocent Sanga wa jimbo Kuu Katoliki la Mbeya.

Kwa mujibu wa Taarifa iliyotolewa na mkurugenzi wa mawasiliano ya Rais Ikulu, Gerson Msigwa imesema Serikali ya Tanzania imeamua kutowazuia watu ndani ya nyumba zao wala kufunga mipaka kwa kutambua madhara makubwa yanayoweza kujitokeza kutokana na kufanya hivyo ndani ya nchi na kwa nchi nane ambazo zinategemea kupata huduma na bidhaa kupitia Tanzania hususani Bandari ya Dar es Salaam.

Amewataka Watanzania wote kuendelea kumuomba Mungu ili aiepushe dunia na janga la ugonjwa wa corona.

Amebainisha kutokana na madhara ya ugonjwa huo duniani, upo uwezekano wa kutokea upungufu wa chakula na kutoa wito kwa Watanzania kuzalisha chakula cha kutosha. Amewataka Watanzania kuendelea kuchapa kazi kila mahali walipo huku wakichukua tahadhari za kutoambukizwa kama wanavyoelekezwa na wataalamu.

Katika ibada hiyo, Magufuli alimshukuru padri huyo kwa mahubiri yaliyowakumbusha Wakristo kuwa msalaba unaokoa na kupitia msalaba Mungu ataiokoa dunia dhidi ya majanga mbalimbali ukiwamo ugonjwa wa corona.