Home | Terms & Conditions | Help

November 26, 2024, 5:29 pm

RAIS MAGUFULI: NINGEWEZA KUWAONGEZEA ELFU TANAO, KESHO BIDHAA ZINGEPANDA BEI

Dar es Salaam: Rais John Magufuli amesema kuwa alikuwa na uwezo wa kuwaongezea wafanyakazi nyongeza ya msharaha hata ya Shilingi elfu tano au elfu kumi kwa kila mfanyakazi wa serekali nchini lakini, alihofia kufanya hivyo kutatibua hali ya kiuchumi nchini na kupelekea bidhaa nyingi kupanda bei.

"Ningeweza kuwaongezea elfu tano tano au elfu kumi, kesho tu bidhaa zingeanza kupanda bei hivyo lazima kwanza tujenge uchumi imara, mimi mwenyewe nilikuwa mwalimu na ndiyo maana nikaenda kuoa mwalimu mwenzangu anayejua shida zetu" amesema Rais Dk. John Magufuli.

Rais Magufuli ameyasema hayo leo May 1 , 2019 katika sikukuu ya wafanyakazi Mei mosi, maadhimisho hayo kwa Tanzania yamefanyika katika uwanja wa Sokoine jijini Mbeya.

Aidha Rais Magufuli amesema haelewi sababu za bodi za mishahara nchini Tanzania kutokutana kwa maelezo kwani yeye hana tatizo na kuonya vikao vyao kutokuwa uchochoro wa kutumia fedha za Serikali vibaya.

“Kwangu mimi hata wakitaka kukutana leo sina shida, sina tatizo namuagiza waziri mwenye dhamana kuhakikisha bodi hizo zinakutana lakini vikao vyao visiwe vichochoro vya kutumia fedha za Serikali vibaya,” amesema Rais Magufuli

“Lazima nitoe angalizo hilo maana unaweza kusikia wameenda kufanya vikao Dubai lakini suala la kukutana na kujadili masuala mbalimbali kati ya wafanyakazi na yale yanayopaswa kutatuliwa mapema nasema kwa dhati sina tatizo mkutane.”

Maadhimisho hayo yamehudhuriwa na Makamu wa Rais Mhe Samia Suluhu Hassan, Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa, Spika wa Bunge Mhe. Job Ndugai, Naibu Spika Dkt. Tulia Ackson, Waziri wa Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Walemavu Mhe Jenista Mhagama na viongozi wa Wafanyakazi

Akizungumzia suala la kushusha viwango vya kodi Rais Magufuli alisema kama waliweza kushusha kutoka asilimia 11 hadi 9 kwa watumishi wa kima cha chini, inawezeka kwa wengine. “Viongozi wa Tucta na wafanyakazi mnapaswa kutambua kuwa Serikali ina sababu ya msingi ya kutofautisha viwango vya kodi kulingana na madaraja ya mishahara,” amesema.