Home | Terms & Conditions | Help

November 25, 2024, 1:35 am

RAIS MAGUFULI AWAPA SIKU 5 WAZIRI KIGWANGALLA NA KATIBU MKUU KUMALIZA TOFAUTI ZAO

Rubondo. Rais wa Tanzania, John Magufuli amewapa siku tano kwa Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk Hamisi Kigwangalla na Katibu Mkuu wa wizara hiyo, Profesa Adolf Mkenda kuondoa tofauti zao vinginevyo atatengua uteuzi wao mara moja.

Rais Magufuli ametoa agizo hilo leo Jumanne Desemba 31, 2019 alipokuwa akizungumza na maofisa na askari wanyamapori na Hifadhi ya Misitu wa Hifadhi ya Taifa ya Kisiwa cha Rubondo ambako ametembelea na kujionea vivutio vya utalii.

Katika salamu zake, Rais Magufuli amelipongeza Shirika la Hifadhi za Taifa (Tanapa) kwa kazi nzuri ya uhifadhi, kukuza utalii na kuchangia mapato ya Serikali lakini ameelezea kusikitishwa kwake na mahusiano mabaya yaliyopo kati ya Waziri Kigwangalla na Profesa Mkenda hali ambayo inasababisha baadhi ya shughuli za wizara kusuasua.

“Ninafahamu watendaji wenu wa juu, katibu mkuu na waziri kila siku wanagombana na ninawatazama taratibu, nilishampa kazi Katibu Mkuu Kiongozi awaite awaeleze lakini wasipobadilika nitawaondoa.”

“Hilo ni lazima nilizungumze kwa dhati, siwezi kuwa na watendaji wa kuteua mimi halafu kila siku wanagombana, kuna mambo mengi hayaendi, Katibu Mkuu hamheshimu Waziri na Waziri naye hataki kwenda na Katibu Mkuu, siwezi kuvumilia hilo,” amesema Rais Magufuli

Kwa hiyo nalizungumza hili siku ya leo tarehe 31 ya mwezi wa 12 (2019) kwamba wajirekebishe na ikiwezekana wajirekebishe ndani ya siku tano, wawe wanasalimiana, wanazungumza, mimi ninafahamu nina vyombo ninajua nani hafai zaidi,” amesisitiza Rais Magufuli.

Aidha, Rais Magufuli ameiongezea muda Bodi ya Tanapa iliyomaliza muda wake chini ya Mwenyekiti Jenerali Mstaafu George Waitara kutokana na kuridhishwa na kazi nzuri zilizofanywa na Tanapa chini ya uongozi wa bodi hiyo ikiwemo kuunda Jeshi Usu la Askari Wanyamapori na Hifadhi ya Misitu, na ametaka Tanapa iendelee kupiga hatua kwa maslahi ya Taifa.

Rais Magufuli amesema Tanzania yenye Hifadhi za Taifa 22, imetoa zaidi ya asilimia 32.5 ya eneo la ardhi yake kwa ajili ya hifadhi na kwamba imefanya hivyo kwa maslahi ya Watanzania na watu wote duniani wanaotembelea hifadhi hizo.