- BREAKING NEWS: TANZANIA YAKANUSHA KUWASHIKILIA KINA DR SLAA NA MWAMBUKUZI
- BREAKING NEWS: RAIS WA MAPINDUZI WA NIGER AMTEUA WAZIRI MKUU MPYA
- BREAKING NEWS: SHILINGI YA KENYA YAPOROMOKA VIBAYA DHIDI YA DOLA
- BREAKING SEREKALI YA RWANDA YAKASIRISHWA NA UBELGIJI KUTOMUIDHINISHA BALOZI WAKE
- BREAKING NEWS: RAIS KIM AKUTANA NA WAZIRI WA ULINZI WA URUSI
RAIS MAGUFULI AFANYA MAZUNGUMZO NA BAADHI YA VIONGOZI WA UPINZANI
Rais wa Tanzania John Pombe Magufuli amekutana na kufanya nao mazungumzo baadhi ya viongozi wa vyama vya upinzani nchini humo katika Ikulu ya jijini Dar es Salaam leo Marchi 3, 2020.
Rais Magufuli amekutana nao Viongozi hao kila mmoja kwa nyakati tofauti tofauti ndani ya Ikulu hiyo.
Wanasiasa hao ni Mshauri Mkuu wa chama cha ACT-Wazalendo Maalim Seif Sharif Hamad, mwenyekiti wa chama cha NCCR-Mageuzi James Mbatia na mwenyekiti wa chama cha CUF, Profesa Ibrahim Lipumba.
Taarifa rasmi ya Ikulu haikueleza undani wa mazungumzo ya viongozi hao na rais licha ya kuchapisha picha za kukutana kwao.
Kupitia Ukurasa wa Instagram, Ikulu ya Tanzania imetoa kipande cha mahojiano na Maalim Seif ambaye hakueleza kwa kina kilichozungumzwa baina yao, akisema kuwa yaliyozungumzwa hawezi kuyaweka hadharani.
"Mimi na mheshimiwa rais tumekutana na kubwa ni kuzungumzia mambo ya nchi yetu, vipi tutaendelea kuifanya Tanzania kuwa nchi ya amani, nchi ya salama, nchi ya upendo kwa watanzania wote," amesema Maalim Seif na kuongeza "Sasa kuna mengine tumezungumza mimi na rais, yamo ndani na huwezi kuyaweka hadharani, ikitokea haja ya kukutana tena tutakutana."
Profesa Ibrahim Lipumba ambaye ni Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF) amempongeza Rais Magufuli kwa ahadi yake kuwa Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu utakuwa huru na wa haki ambapo pia amepongeza juhudi kubwa zinazofanywa na Serikali kupambana na rushwa, kudhibiti matumizi ya Serikali, kulinda na kutumia vizuri rasilimali za Taifa, kuboresha elimu na kuimarisha uchumi.
Lipumba ametoa wito kwa Watanzania wote kuweka uzalendo mbele, kudumisha amani na utawala bora na amewataka wanachama wote wa CUF kujiandaa kushiriki Uchaguzi Mkuu utakaofanyika baadaye mwaka huu kwa kufuata taratibu na sheria zilizopo.
Kwa upande wake Mbatia amewataka wanasiasa kuacha kukamiana na kuchochea mambo hasi dhidi ya Taifa na badala yake waungane kuendeleza mambo mazuri
yanayofanywa na Serikali ikiwemo kuboresha elimu, upatikanaji wa nishati na mengine yenye maslahi mapana kwa wananchi. Mbatia ametoa wito kwa wanasiasa na Watanzania wote kwa ujumla kuweka mbele maslahi ya Taifa badala ya kukumbatia mambo yenye maslahi binafsi na ameipongeza Serikali kwa kufanya vizuri katika maeneo mbalimbali.
Mazungumzo hayo baina ya Magufuli na wapinzani yanakuja ikiwa Tanzania inaelekea kwenye uchaguzi mkuu mwaka huu.
Vyama vya upinzani nchi Tanzania vimekuwa vikimkosoa Magufuli na utawala wake kwa kuwaminya.
Vyama hivyo vimezuiliwa kufanya mikutano ya hadhara isipokuwa kwa wawakilishi wa maeneo kama wabunge.
Juma lililopita, vyombo vya habari nchini humo viliripoti kuwa Mwenyekiti wa Chadema alikamatwa (na baadaye kuachiliwa) akihutubia mkutano wa hadhara jimboni kwake licha ya kuwa na kibali kwa kuwa alizungumzia kuhusu Tume ya Uchaguzi.