Home | Terms & Conditions | Help

November 24, 2024, 1:47 pm

RAIA WA CAMEROON AHUKUMIWA KULIPA FAINI YA MILIONI 100 KWA KUSAFIRISHA PESA

Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es salaam imemuhukumu kijana mmoja raia wa Cameroon Kohnson Tebo (32) kulipa faini ya Sh milioni 100 ama kwenda jela kwa miaka mitatu baada ya kukiri shitaka moja la kusafirisha fedha bila ya kuzitolea taarifa.

Pia Mahakama imeamuru kutaifishwa kwa USD 84,300 alizokutwa nazo mshtakiwa.

Hukumu hiyo imesomwa na Hakimu Mkazi Mwandamizi, Rashidi Chaungu baada ya mshtakiwa kukiri kosa lake.

Kabla ya kusomwa kwa hukumu hiyo Wakili wa Serikali Mkuu, Shadrack Kimaro aliomba mahakama pamoja na adhabu ya kulipa faini aliomba fedha zitaifishwe kuwa mali ya Serikali.

Mapema akimsomea mshtakiwa kosa lake, Wakili wa Serikali Mwandamizi, Wankyo Simon alidai Februari 27 mwaka huu katika Uwanja Ndege wa Julius Nyerere uwanja namba tatu, mshtakiwa alikutwa akiondoka nchini huku akiwa na USD 84,300 bila kuzitolea maelezo kwa Mamlaka ya Forodha ya Jamhuri ya Muungano ya Tanzania.

Aidha mshtakiwa alisomewa maelezi ya awali ambapo anadaiwa, kwa mujibu wa kumbukumbu zilizopo Mamlaka ya Forodha, wakati anaingia nchini hakueleza kama anaingia na fedha zozote na kwamba Februari 27 alikuwa akiondoka nchini kupitia ndege ya Rwanda na alikuwa na tiketi ya kielekitroniki pamoja na pasi ya kusafiria.

Ndege hiyo ilikuwa ikiondoka saa 11.40 jioni kuelekea Kigali na baadae Duoala Cameron.

Imedaiwa Mshtakiwa huyo mkononi alikuwa ameshikilia begi, akiwa uwanjani mshtakiwa alianza utaratibu wa kuingia na akapita kwenye mashine ya kwanza ya ukaguzi , alipoenda kwenye mashine ya pili ili aingie kwenye chumba cha kusubiria abiria , kitu kisicho cha kawaida kiligundulika katika begi lake.

Imedaiwa alielekezwa aache mkoba wake kwenye mashine kwa mara ya pili ambapo kitu kisichocha kawaida kilibainika.

"Aliamuliwa kutoa kila kitu kilichokuwa kwenye begi , fedha hazikuwa miongoni mwa vitu vilivyotolewa.... Wakati begi tupu lilipowekwa kwenye mashine ilibaika kuwa ndani ya begi kwa achini zilifichwa fedha..Sehemu hiyo ilipopekuliwa ilibainika USD 84,300 zilifichwa,"alidai Wankyo.

Amedai fedha zilizokamatwa zimewekwa kwenye akaunti katika Benki ya NMB na namba zake zilinakiliwa.

Inadaiwa kumbukumbu za uhamiaji zinaonesha kuwa mshtakiwa aliingia nchini Februari 26, 2020 kama mtalii na kupewa viza ya utalii, hakutembelea kituo chochote cha utalii na alipoingia nchini hakueleza kama alikuwa na fedha za Marekani.

Ushahidi ulikua unaonesha wazi kuwa mshtakiwa alikuwa anaondoka nchini bila kueleza Mamlaka ya Forodha fedha alizokuwa nazo.