- BREAKING NEWS: TANZANIA YAKANUSHA KUWASHIKILIA KINA DR SLAA NA MWAMBUKUZI
- BREAKING NEWS: RAIS WA MAPINDUZI WA NIGER AMTEUA WAZIRI MKUU MPYA
- BREAKING NEWS: SHILINGI YA KENYA YAPOROMOKA VIBAYA DHIDI YA DOLA
- BREAKING SEREKALI YA RWANDA YAKASIRISHWA NA UBELGIJI KUTOMUIDHINISHA BALOZI WAKE
- BREAKING NEWS: RAIS KIM AKUTANA NA WAZIRI WA ULINZI WA URUSI
NEWS:SERIKALI,WASHIRIKI WA MAENDELEO KUFANYA MAZUNGUMZO YA UJENZI WA UZIO HIFADHI YA SERENGETI
DODOMA: SERIKALI imesema inafanya mazungumzo na Washirika wa maendeleo ili kuangalia namna ya kuweka uzio wa kilomita 140 katika Hifadhi ya Taifa ya Serengeti ili kukabiliana na tatizo la wanyama waharibifu wa mazao.
Waziri wa Maliasili na Utalii, Prof.Jumanne Maghembe bungeni jana alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Bunda mjini(chadema), Ester Bulaya.
Bulaya alitaka kujua serikali ina mkakati gani wa kumaliza tatizo la Wanyamapori ambao wamekuwa wakivamia kwenye mashamba ya wakulima hasa kipindi cha mavuno kwenye maeneo mbalimbali yenye Hifadhi za Taifa ikiwemo wilaya ya Bunda na kusababisha njaa kwa wananchi.
Akijibu swali hilo, alikiri katika Mkoa wa Mara na hasa Wilaya za Bunda, Serengeti, Tarime na wilaya za maeneo ya Hifadhi hiyo yamekuwa yakikabiliwa na adha kubwa sana ya wanyama waharibifu.
“Wanyama hawa wamekuwa wakitokea katika Hifadhi ya Taifa ya Serengeti na kuingia katika mashamba ya watu hasa wakati wa mavuno ndio kadhia hii inaongezeka,”alisema Waziri huyo
Hata hivyo alisema kwa mwaka huu Wizara imechukua hatua za muda mfupi kwa kuongeza askari na magari ya doria ili kuhakikisha wanaokoa wananchi kwenye tatizo hilo.
“Tunazungumza na washirika wetu wa maendeleo kuona ni kwa namna gani tunaweza kuweka uzio wa kilomita 140 kwa majaribio ili kuangalia kama itakuwa ni suluhisho la tatizo hili,”alisema Waziri huyo.
Awali, Katika swali la msingi la Mbunge wa Ulanga(CCM), Goodluck Mlinga alitaka kujua serikali ina mpango gani wa kuzuia uharibifu huo wa mazao katika mashamba ya Kata za Ruaha, Chilombola, Ilonga, Ketaketa, Mbuga ya Lukande na Lupilo ambayo yamekuwa wakivamiwa na wanyama kama vile Viboko na Tembo.
Prof.Maghembe akijibu swali hilo alisema kumekuwepo na ongezeko la wanyamapori wakali na waharibifu katika maeneo mbalimbali nchini yakiwemo ya kata hizo.
“Kutokana na madhara yanayosababishwa na wanyamapori hususan Tembo na Viboko, serikali inaendellea kuchukua hatua mbalimbali katika kunusuru maisha na mali za wananchi,”alisema
Alitaja hatua hizo kuwa ni pamoja na kufanya doria za wanyamapori wakali na waharibifu ili kudhibiti madhara ya wanyama hao kwa kutumia askari waliopo pori la Akiba la Selous.
Alisema pia kutoa elimu ya uhifadhi kwa jamii kujikinga na wanyamapori wakali na waharibifu, kuendeleza mbinu mbalimbali za kupunguza madhara yanayotokana na uvamizi wa tembo na kukuza kipato na pia kutumia ndege zisizokuwa na rubani kwa ajili ya kufukuza tembo pindi wanapovamia mashamba au makazi.