Home | Terms & Conditions | Help

November 27, 2024, 9:46 am

NEWS:MAHAKAMA YATUPILIA MBALI KESI YA VYAMA 10 VYA UPINZANI

Dar es Salaam: Mahakama Kuu ya Tanzania leo juamatatu 142019 imetupilia mbali shauri la Kikatiba la kupinga Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria ya Vyama vya Siasa wa Mwaka 2018, lililokuwa limefunguliwa na vyama 10 vya upinzani hapa nchini.

Uamuzi huo umetolewa na Jaji Benhajj Masoud, baada ya kukubaliana na hoja za pingamizi la Serikali, kuwa shauri hilo halikuwa halali kuwepo mahakamani kwa kuwa lilikiuka utaratibu na sheria.

Shauri hilo la Kikatiba namba 31 la mwaka 2018 lilifunguliwa Mahakama Kuu, Masjala Kuu na wanasiasa watatu akiwemo Kiongozi wa Chama cha ACT- Wazalendo, Zitto Kabwe, kwa niaba ya muungano wa vyama 10 vya upinzani, dhidi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG).

Wengine ni kaimu katibu mkuu Bara wa Chama cha Wananchi (CUF), Joran Bashange na Mkurugenzi wa Habari, Uenezi na Mahusiano CUF, Salim Bimani wote kutoka kambi ya Katibu Mkuu, Seif Sharif Hamad.

Wanasiasa hao walikuwa wakipinga kifungu cha 8 (3) cha Sheria ya Utekelezaji wa Haki za Msingi kinachozuia muswada kupingwa mahakamani.

Pia walikuwa wakipinga muswada huo wakidai unakiuka haki za Kikatiba za kisiasa kwani unazifanya shughuli mbalimbali za kisiasa kuwa jinai na unampa mamlaka makubwa Msajili wa Vyama vya Siasa kuingilia mambo ya ndani ya vyama hivyo yakiwemo ya uongozi.

Serikali iliweka pingamizi ikiiomba mahakama hiyo ilitupilie mbali, huku ikiwasilisha jumla ya hoja kumi.

Hata hivyo, Jaji Masoud katika uamuzi wake wa kutupilia mbali shauri hilo amezingatia hoja mbili tu kati ya hizo kumi, ambazo zimetosha kulitupilia mbali.

Hoja hizo za pingamizi la Serikali ambazo Jaji Masoud amezizingatia ni pamoja na hoja ya tatu ya pingamizi la Serikali kuchanganya maombi mawili katika shauri moja na sehemu ya hoja ya nane kwamba shauri hilo linakiuka sheria.

Jaji Masoud amesema walalamikaji hawakupaswa kuomba Mahakama itamke kifungu cha 8(3) cha Sheria ya Haki za Msingi na Wajibu kinakiuka Katiba wakati huohuo wanaomba pia mahakama itamke kuwa muswada huo unakiuka katiba.

Amesema maombi hayo mawili yanategemeana, kwani ombi la pili la muswada linategemea uamuzi wa ombi la kwanza la kupinga kifungu hicho cha sheria na kwamba walipaswa kwanza wafungue shauri katika ombi la kwanza na kama wangekubaliwa ndipo wangefungua shauri la kupinga muswada.

Katika hoja nyingine Jaji Masoud amesema kwamba shauri hilo linakiuka kifungu cha 8 (2) cha Sheria ya Haki za Msingi na Wajibu, kwani hawakufuata utaratibu unaoelekezwa katika kifungu hicho.

Kifungu hicho kinaelekeza mtu yeyote anayedai haki zake zinakiuka au zinaelekea kukiukwa anapaswa kutafuta nafuu kwa kutumia njia nyingine zilizopo kwanza kabla ya kwenda mahakamani.