Home | Terms & Conditions | Help

November 25, 2024, 3:50 am

NEWS:LISSU KUBURUZA SPIKA WA BUNGE MAHAKAMANI

DODOMA: MWANASHERIA Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Tundu Lissu, amesema Mbunge wa Kawe, Halima Mdee, John Mnyika wa Kibamba na yule wa Bunda, Ester Bulaya, wamepeleka ombi kwenye Mahakama Kuu Kanda ya Dodoma, kuomba kumshtaki Spika wa Bunge, Job Ndugai na Mwenyekiti wa Kamati ya Maadili, Haki, Kinga na Madaraka ya Bunge, George Mkuchika.

Amesema kesi hiyo wanataka kuifungua kutokana na kutoridhishwa na adhabu zilizotolewa kwa wabunge hao na kuwa, zipo kinyume na kanuni za Bunge.

Vilevile, Lissu amesema kambi ya upinzani imepata taarifa ya kutaka kukamatwa kwa Mbunge wa Tarime Vijijini, John Heche, kutokana na kuwataka wananchi walinde rasilimali zao baada ya Rais kusema mgodi wa Acacia hauna kibali cha kuchimba dhahabu nchini.

Akizungumza na Waandishi wa Habari leo Mjini hapa,Lissu amesema wameamua kupeleka maombi kwenye mahakama kuu ya kuomba kumshtaki Spika Ndugai pamoja na Mwenyekiti wa Kamati ya Maadili Mkuchika sababu zikiwa ni kupinga Uamuzi wa Spika wa kuwasimamisha Mdee, Bulaya na Mnyika kutohudhuria vikao.

‘Hawa viongozi wetu watatu wamepeleka maombi ili mahakama kuu iweze kutoa amri ya kufutilia mbali uamuzi wa Spika wa Bunge letu wa kumsimamisha Mheshimiwa John Mnyika kwa vikao saba vya bunge hili la saba’’

‘’Pia mahakama kuu iweze kufuta kabisa uamuzi wa Bunge wa kuwasimamisha kuhudhuria vikao vilivyobaki vya bunge hili vikao vyote vya bunge la nane na vikao vyote vya bunge la tisa waliowasimamisha Halima Mdee na Ester Bulaya’’

Amesema sababu nyingine ya kupeleka ombi Mahakamani ni hoja ya uamuzi wa Spika ulikuwa na upendeleo kwa kuwanyima haki wabunge wa upinzani na kuwapendelea Wabunge wa Chama cha Mapinduzi(CCM).

‘’Spika kwa maneno aliyoyasema bungeni kwamba hawa waheshimiwa siku ya Jumatatu ni adhabu tu Spika huyo huyo siku ya Jumatatu akawa ndio Jaji wa hilo shauri huwezi kuwa jaji katika shauri lako mwenyewe inaonesha dhahiri kulikuwa na upendeleo’’alihoji Lissu.

Lissu alisema sababu nyingine ya kupeleka ombi hilo ni kuwa kulikuwa na ukiukwaji mkubwa wa taratibu katika kikao hicho cha bunge.


‘’Pia tumeenda ili tuweze kujua Je Mamlaka ya Bunge ya kumsimamisha Mbunge yana ukomo, Je Bunge linaweza likaamua likamsimamisha Mbunge kwa vikao vyote Ishirini hapa tunataka tujue ili liwekwe wazi’’alisema

Akilizungumzia suala la kutaka kukamatwa na Jeshi la Polisi kwa kudaiwa kuwahamasisha Wananchi waende kuvamia Mgodi wa Acacia,Heche alisema haogopi mtu yoyote na yupo tayari kukamatwa kwani anaamini Wananchi wake walikuwa sahihi.

‘’Nasema kwa kurudia tenana naendelea kukaa humu ndani kwa sababu hawawezi kunikamata, humu ndani lakini naendelea kujiuliza nikae humu ndani kwa kumuogopa nani kama wao wanataka kunikamata nipo tayari nitatoka na sitakaa humu waje tu kunikamata siogopi mtu yoyote’’alisema

Heche alisema Wananchi wa Tarime matatizo makubwa nakuna watu wameuwawa huku wengine wakibaki kuwa wajane lakini serikali imekuwa haiwasikilizi.

‘’Mimi wamenituma nije niwasemehe hapa na narudia tena kama Rais amesema watu wa Acacia ni wezi naanzaje kusema wale sio wezi kama wanataka kusema sio wezi mbona Rais kasema ni wezi kama Rais na tume wamesema mimi naanzaje kupinga.

‘’Narudia kusema Acacia ni wezi na wananchi wana haki ya kuwaarest wezi na wananchi wa Tarime wanachotaka ni kulipwa haki zao kama watu wa kamawaida wanalia kuhusiana na wizi, Je hawa wanaoishi migodini watakuwa na hali gani’’alisema