Home | Terms & Conditions | Help

November 26, 2024, 3:41 pm

NEWS: ZITTO AWAVURUGA WAZIRI MPANGO NA NAIBU WAKE DKT KIJAJI

Mbunge wa Kigoma Mjini, Zitto Kabwe (ACT-Wazalendo) jana alizua hoja nzito kwa Waziri wa Fedha na Mipango Dkt Philip Mpango na Naibu wake Dk. Ashatu Kijaji, alipodai kuwa uchumi wa Tanzania unaporomoka licha ya serikali ya awamu ya tano kutumia Sh. trilioni 18.7 kuboresha miundombinu nchini.

Mchuano wa Zitto na Mawaziri hao ulikuwa wakati wa mjadala wa hotuba ya makadirio ya bajeti ya Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano kwa mwaka ujao wa fedha. Katika hoja yake , Kiongozi huyo wa ACT-Wazalendo alisema katika kipindi cha miaka minne, Wizara ya Ujenzi imechukua asilimia 46 ya bajeti yote ya maendeleo, lakini haijatoa matokeo ya kuridhisha kwenye ukuaji wa uchumi.

“Mheshimiwa Naibu Spika, jumla ya fedha ambazo tumeziingiza kwenye wizara hii ni Sh. trilioni 18.7 sawa na asilimia 46 ya jumla ya fedha za bajeti ya maendeleo ya nchi ambayo ni Sh. trilioni 40.6. “Kwa hiyo, asilimia 46 ya bajeti ya maendeleo unaishika wewe Kamwelwe na manaibu wako wawili.

Wabunge wana haki ya kuuliza, kiasi hiki cha fedha ambacho tulichokiingiza kwenye wizara hiyo mpaka sasa kimezalisha viwanda vingapi? "Tunazungumza kuhusu namna ambavyo fedha ambazo tunameingiza kwenye miradi kama reli, ndege, zinachocheaje sekta nyingine za uchumi? "Tungepata maelezo ya serikali hapa, kwamba tumeingiza Sh. trilioni 18.7 na matokeo yake ni nini? Waziri Mpango analijua sana hili, kwamba moja ya sekta zinazopaswa kuonyesha zilivyochangia uchumi ni ujenzi.

“Kwanini sisi ambao tunaingiza fedha nyingi kiasi hiki, na bado kasi ya ukuaji wa uchumi iwe ni ndogo? Leo hii tunabishania makisio ambayo IMF wameyatoa ya asilimia nne na kadhalika. "IMF na Waziri Mpango hawajakanusha makisio haya, wamekanusha 'leaked report' (ripoti iliyovuja) lakini makisio bado ni yale yale. Hata ukichukua makisio ya serikali ya asilimia sita, lakini 'before' (kabla) serikali ya awamu ya tano iingie madarakani 'economy' (uchumi) yetu ilikuwa inakua kwa asilimia 'for 10 years' (kwa miaka 10).

"Tangia serikali ya awamu ya tano imeingia madarakani, Sh. 18 trilioni zimeingizwa kwenye 'construction' (ujenzi) lakini 'sector growth rate' (kasi ya ukuaji wa kisekta) iko chini, kwa nini? Zitto alihoji. Alitolea mfano nchi ya Kenya kwamba imejenga reli ya kisasa kwa mkopo mkubwa, lakini sekta yao ya ujenzi imekua kwa asimilia 1.5.

“Hata mkiacha ile asilimia nne ya IMF, twendeni na ile ya serikali ya asilimia sita, ni kwa sababu mipango yetu ya maendeleo ya miundombinu ni kutoa fedha kwenda nje na hatuingizi ndani na ndiyo maana mzunguko wa fedha ni mdogo sana, mmewapa kazi makandarasi wa nje, wanaagiza malighafi zote kutoka nje," Zitto alisema.

Aliongeza: "Mnakusanya kodi kwa muuza nyanya kumlipa Mturuki, naye anapeleka Uturuki ndiyo maana uchumi haukui, hata mjenge hoja namna gani, nimeona ile ya serikali kwenda IMF, kusema tuna makisio ya miradi mikubwa haya ni makosa, tuna SGR, Stiegler’s Gauge, miradi yote hii haina maana, 'all the money' (fedha zote) zinaenda nje na huduma yetu ya deni la taifa ni kubwa." Kauli hiyo ilimwinua kitini Waziri Mpango akiomba kumpa taarifa Zitto,

Mpango alisema: "Nataka nimpe taarifa Mheshimiwa Zitto, hapa nimeshika ripoti ya rasmi ya pato la taifa na ukuaji wake za 2018 ambayo iko bayana. "'Growth rate' (kasi ya ukuaji) ya 2013 ilikuwa asilimia 6.8, 2014 ilikuwa asilimia 6.7, 2015 asilimia 6.2, 2016 asilimia 6.9, 2017 asilimia 6.8 na 2018 ilikuwa silimia 6.9, sasa hiyo 'growth rate' iliyoteremka ni ipi? “Kwanini mnatumia taarifa za IMF ambazo hazina ukweli"? Na niliwaambia katika Bunge hili kwamba bado tunazungumza na African Development Bank 'wana-project' (wanadiria) uchumi wa Tanzania 2019 utakua kwa asilimia 6.8, makadirio ya World Bank (WB) ni asilimia 6.6, sasa hiyo growth rate iliyoteremka ni ipi?" Dk. Mpango alihoji.

Baada ya taarifa hiyo, Naibu Spika, Dk. Tulia Ackson, alimuuliza Zitto kama anaipokea taarifa hiyo na mbunge huyo akasema: “Naipokea taarifa ya Waziri Mpango, ninachotaka kumwambia; kwanza waziri anajua kwamba mamlaka ya 'economic surveillance' (tathmini ya kiuchumi) ya dunia ni moja, nayo ni IMF na anafahamu kwa sababu amefanya kazi huko.

"WB, African Development Bank na hata Wizara yetu ya Fedha makisio wanayoyatumia ni ya IMF, siyo makisio mengine na anafahamu, labda atakataa kwa sababu anaitetea serikali hapa," Zitto alisisitiza. Kutokana na kauli hiyo ya Zitto, Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Kijaji alisimama na kutoa ufafanuzi kuwa matokeo ya kupeleka fedha kwenye sekta ya ujenzi, yanaonekana baada ya muda mrefu.

Baada ya kuruhusiwa kuendelea kuchangia mjadala huo, Zitto alisema: "Kuna tofauti kubwa sana kati ya kasi ya ukuaji wa uchumi na uchumi. Sekta ya ujenzi ni ya pili kwenye kasi ya ukuaji, si ya pili kwenye uchangiaji wa kisekta.

"Lakini pointi yangu hapa, wastani wetu tuliokuwa nao ni asilimia. Dk. Mpango anajua panapokuwa na mdororo wowote wa uchumi, serikali inaingiza fedha kwenye mzunguko.

"Na kwa miaka mitatu iliyopita, tumeingiza Sh. 18.7 trilioni kwenye ujenzi, naomba nijibiwe, hii fedha ambayo tumeipampu, imezalisha viwanda vingapi, ajira za kudumu ngapi, sekta ya kilimo imechochewa vipi? Zitto alihoji.