Home | Terms & Conditions | Help

November 26, 2024, 7:35 pm

NEWS: ZITTO ATAKA UKAGUZI WA SH TRIL 1 ZILIZOTUMIKA KUNUNUA NDEGE

Mbunge wa Kigoma Mjini Zitto Kabwe amemuomba Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serekali kufanya ukaguzi maalumu wa kiasa cha fedha cha Shilingi Trilioni 1 zilizotumika kununua ndege za shirika la ndege la Tanzania (ATCL)

"Tunamwomba CAG 1) Afanye Ukaguzi Maalumu wa Fedha za Umma Sh. 1Tril zilizotumika kununua ndege 2) Afanye Ukaguzi wa usimamizi wa mkataba wa ukodishwaji wa ndege hizo kati ya Wakala wa ndege za Serikali na ATCL ili Watanzania wajue matumizi sahihi ya Fedha zao za Kodi" amesema Zitto

Akizungumza na waandishi wa habari leo Jumamosi April 14, 2019 mkoani Dodoma, Zitto ambaye ni Kiongozi mkuu wa chama cha ACT Wazalendo amesema kuwa chama hicho kimeisoma, kuipitia na kuichambua taarifa CAG, kwa lengo la kuitumia ili kuwasaidia kutimiza wajibu wa chama katika kuisimamia Serikali kama chama mbadala nchini na kama Chama cha Upinzani Bungeni.

Zittoa alianza kuichambua Ripoti hiyo katika vipengele mbalimbali kwa lugha Rahisi kwa mwananchi wa kawaida

amesema “Kwenye bajeti ya mwaka wa fedha wa 2016/17, ambayo ni bajeti ya kwanza ya Serikali ya awamu ya tano, mipango ya Serikali ilikuwa ni kukusanya shilingi 29.5 trilioni, kwa mujibu wa ripoti ya CAG ya 2016/17, kati ya fedha hizo, Serikali ilikusanya shilingi 25.3 trilioni. Na hivyo, kutokufikia lengo la makusanyo kwa 14.33%, kwenye uchambuzi wetu wa mwaka jana tulieleza kuwa bajeti za Serikali si halisia.”

Zitto amesema kwenye ripoti ya mwaka 2017/18, kwa mara nyengine, CAG amelithibitishia Taifa kuwa Serikali ya awamu ya tano inatunga bajeti ambayo sio halisia. Katika Bajeti ya Serikali ya mwaka wa fedha wa 2017/18 jumla ya Sh. 31.7 trilioni zilitarajiwa kukusanywa na zilipitishwa kutumika na Bunge. Hata hivyo, kwa mujibu wa ripoti hii ya CAG, Serikali iliweza kukusanya kutoka vyanzo vyake vyote Sh. 27.7 trilioni tu, na kutumia shilingi 26.9 trilioni. Hivyo ikikosa makusanyo kwa 12.66% na ikikosa matumizi kwa 15.2%.

“Kwa miaka mitatu ya mwisho ya Serikali ya awamu ya nne, wastani wa lengo lisilofikiwa na Serikali katika ukusanyaji wa mapato ya Bajeti ni tarakimu moja, 6.3% tu, ambapo kwa mwaka 2013/14 lengo halikufikiwa kwa 9%, kwa mwaka 2014/15 nako lengo halikufikiwa kwa 4%, na kwa mwaka wa fedha wa 2015/16 lengo halikufikiwa kwa 6% tu.

“Hii inadhihirisha Kwa mara nyengine tena kuwa Serikali ya Awamu ya Tano hutangaza viwango vikubwa vya Bajeti ili kufurahisha umma ilhali uhalisia ni kuwa Bajeti ni ndogo zaidi. Kwa miaka 2 mfululizo CAG ametuonyesha kuwa Serikali inashindwa kufikia makadirio ya Bajeti Kwa zaidi ya shilingi Trilioni 4 kutoka Bajeti inayopitishwa na Bunge,” amesema.

Zitto amesema katika ukurasa wa 91 wa ripoti ya CAG ya mwaka wa fedha wa 2017/18, CAG anasema, nanukuu “Ikilinganishwa taarifa ya kutoa fedha (exchequer issue report) na taarifa ya Fedha zilizopokelewa na kuripotiwa katika taarifa za fedha za Mafungu husika pamoja na barua za kukiri mapokezi ya fedha kutoka Wizara ya Fedha na Mipango, imebaini utofauti wa taarifa zilizoripotiwa.”

CAG ameeleza kuwa tofauti hiyo imesababishwa na kutokuwepo kwa mifumo thabiti ya usuluhishi kati ya fedha zilizotolewa na hazina na fedha zilizotolewa na wahisani wa maendeleo moja kwa moja kwenye miradi ya maendeleo katika Wizara.

“Ni muhimu sana kusisitiza hapa kuwa kwa mujibu wa CAG kuna fedha shilingi trilioni 4.8 ambazo makusanyo yake hayakuingizwa mfuko mkuu wa Serikali (tazama uk 91 wa Taarifa, tanbihi namba 15),

“Suala la udhaifu wa mifumo katika hazina pia limeelezwa kwa kina Katika Taarifa ya CAG ya Uhakiki wa Tofauti ya shilingi 1.5 Trilioni Katika mwaka wa Fedha 2016/17. Bado udhaifu huu unaendelea na madhara yake Katika usimamizi wa Fedha za Umma ni makubwa sana,” amesema.