Home | Terms & Conditions | Help

November 24, 2024, 4:52 pm

NEWS: ZITTO AKUTWA NA KESI YA KUJIBU

Dar es Salaam. Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Jijini Dar es Salaam nchini Tanzania imemkuta na kesi ya kujibu, Mbunge wa Kigoma Mjini na Kiongozi Mkuu ACT- Wazalendo Zitto Kabwe.

Uamuzi huo umetolewa leo Jumanne, Februari 18, 2020 na Hakimu Mkazi Mkuu wa Mahakamani hiyo, Huruma Shaidi baada ya kupitia majumuisho ya pande zote mbili yaliyowasilishwa mahakamani hapo.

Zitto ambaye amerejea nchini Jana akitokea Marekani anakabiliwa na mashtaka matatu yote ya uchochezi, anayodaiwa kuyatenda Oktoba 28 mwaka 2018 katika mkutano na waandishi wa habari uliofanyika ofisi za makao makuu ya chama cha ACT Wazalendo.

Katika shtaka la kwanza, inadaiwa siku hiyo akiwa katika mkutano na waandishi wa habari kwa nia ya kuleta chuki miongoni mwa wananchi wa Tanzania dhidi ya Jeshi la Polisi alitoa maneno ya uchochezi.

Alitoa maneno ya uchochezi kuwa "watu ambao walikuwa ni majeruhi katika tukio la mapambano baina ya wananchi na polisi, wakiwa wamekwenda hospitali kupata matibabu katika kituo cha afya cha Nguruka, polisi wakapata taarifa kuwa kuna watu wanne wamekwenda hospitali kituo cha afya Nguruka kupata matibabu wakawafuata kule wakawaua."

Baada ya kukutwa na tuhuma za kujibu, Zitto ameieleza mahakama kwamba atakuwa na mashahidi kumi na atatoa ushahidi wake kwa kiapo.

Upande wa mashtaka tayari umetoa mashahidi 15 katika kesi hiyo.

Hakimu Shaidi ameahirisha kesi hiyo hadi Machi 17, 18,19 na 20 mwaka 2020 ambapo mshtakiwa atanza kujitetea.