Home | Terms & Conditions | Help

November 25, 2024, 9:56 pm

NEWS: WIZARA YASHUTUMIWA KUMDHULUMU MSHINDI WA UFUGAJI DODOMA

DODOMA: Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi imedaiwa kumdhulumu mfugaji Mshandoo Parutu wa kata ya Chitego Wilayani Kongwa sh 1.5 milioni aliyeibuka kidedea katika mashindano ya kitaifa ya ufugaji bora mwaka jana.


Mshandoo alifikisha malalamiko hayo kwa Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi, Dk Charles Tizeba leo wakati wa mashindano ya mifugo katika viwanja vya Nanenane Nzuguni mjini hapa.

"Nimetumia Sh 300,000 kufuatilia zawadi yangu hiyo baada ya kushinda mashindano hayo bila mafanikio. Kwa mkuu wa Wilaya ya Kongwa (Deo Ndejembi) nimeenda mara tatu ofisini kwake. Nimeenda pia kwa ofisa mifugo wa wilaya ambaye aliniambia wahusika wa zawadi hizo ni wizara,"alisema.

Amesema alipokwenda mara ya mwisho aliambiwa kuwa kuna mfugaji alishapewa zawadi mfugaji mwingine wa wilayani kwake.

" Jibu la mwisho nililopewa kuwa mhusika anastaafu kwa hiyo aachwe andelee kushughulikia mambo yake,"alisema.
Mashandoo alisema kuzungushwa kupata zawadi hiyo kumemfanya akate tamaa ya kushiriki katika maonyesho ya mwaka huu ingawa ana ngombe ambao wanaubora mkubwa kuliko mwaka jana.

Amesema juzi alipata wazo la kufika katika viwanja vya Nanenane kuonana na waziri ili kuwasilisha malalamiko yake.

"Kwa maneno ya waziri Jumatatu nitajaribu kufuatilia tena zawadi yangu, nadhani sasa nitapata. Amesema akipata zawadi yake mwakani atashiriki tena katika mashindano hayo,"alisema.

Mkuu wa Wilaya ya Kongwa, Deogratus Ndejembi amesema mfugaji huyo alikuja mwaka jana katika maonyesho kupitia halmashauri ya Wilaya ya Kongwa na kushinda mashindano hayo.

"Mfugaji huyu ameshakuja zaidi ya mara mbili kudai fedha zake ama mtamba wa ng'ombe kama zawadi zilivyoainishwa katika mashindano hayo," alisema na kuongeza kuwa kushindwa kupata kwa zawadi hiyo kumemfanya kukata tamaa ya kushiriki mashindano hayo mwaka huu.

Akizungumzia suala hilo.Dk Tizeba amewaagiza maofisa wa wizara hiyo wamlipe mfugaji huyo fedha zake.

"Mmulipe mfugaji huyu na hawa wa leo msiwakope muwalipe," amesema Dk Tizeba katika maahindano hayo ambayo mshindi atatangazwa katika kilele cha maonyesho hayo Jumatatu.