Home | Terms & Conditions | Help

November 26, 2024, 11:17 pm

NEWS: WAZIRI WA KILIMO ATISHIA KUUFUTA WAKALA WA NFRA.

DODOMA: Waziri wa Kilimo Japhet Hasunga ametishia kuufuta Wakala wa Hifadhi ya Chakula nchini(NFRA), kama hautakuwa na uwezo wa kununua tani laki tano za mazao kwa wakulima.

Hasunga ameyasema hao leo Jijini Dodoma wakati akizindua mashine maalum ya kusafisha mahindi iliyotolewa na Mpango wa Chakula Duniani(WFP) kwa NFRA.

Akiendelea mbele Zaidi ameongeza kuwa “Hilo sikubaliani nalo, nategemea mnunue mazao kwa wananchi, mnasema hamna mtaji wakati mnao, nunua uza, nunua uza…Hapa mnajifanya mpo ‘busy’ kwa hizo tani 36,000 za WFP hapana mnatakiwa kufanya kazi zaidi,”.

“Mtafute maghala mazuri kama Marekani wanaweza kutunza kwa miaka 10 hadi 15 kwanini sisi?, jambo la tatu lazima mbadili mfumo wa ununuaji nafaka, mfumo mnaotumia una gharama kubwa, kuna mifumo mizuri ipo ya kielektroniki,”amesema.

Hasunga amesema kama wasipopunguza gharama za uendeshaji atawaondoa huku akitolea mfano gharama za usafirishaji kwa gunia moja ni Sh.7500 wakati watu binafsi wanasafirisha kwa Sh.3000 hadi 2000.

Hasunga amesema kuwa mashine hiyo ina thamani ya Sh.Milioni 399.8 na itakuwa na uwezo wa kusafisha tani 100 kwa siku za mahindi.

“Nashukuru WFP kwa mashine hii lakini naomba muangalie uwezekano wa kutusaidia pia kwenye kanda zetu zingine,”amesema.

Hasunga amesema kilimo kina changamoto nyingi hivyo inahitajika kupata teknolojia ya kuboresha kilimo na kubadili kilimo kutoka kilimo cha kujikimu na kuwa kilimo cha biashara.

Kaimu Mtendaji wa NFRA Vumilia Zikankuba amesema wamekuwa wakishirikiana kwa muda mrefu WFP na mikakati wanayoifanya imesaidia serikali.

“Miongoni mwa mikakati ni kuboresha miundombinu ya kuhifadhi kwa kutumia teknolojia kwenye uhifadhi kwa kuwa kila siku teknolojia inabadilika,”Amesema.

Amesema zoezi la kuuza tani 36,000 kwa WFP linaendelea hadi sasa wamechukua tani 20400.

“Tupo tayari kuwauzia kadri watakavyohitaji na yatakuwa na ubora unaotakiwa,tunakuhakikishia Waziri hatutakuangusha katika soko lolote la kimataifa tutaendelea kuwauzia mazao yenye ubora,”amesisitiza.

Kwa upande wake Mwakilishi wa WFP Tanzania, Michael Danford amesema WFP inaangalia namna ya kumtoa mkulima katika kilimo kidogo na kuwa na kilimo kikubwa.

Amesema dola za Marekani milioni 330 zimeingizwa nchini Tanzania na tangu mwaka 2010 zimenunuliwa tani 500,000 za chakula, kati ya hizo tani 200,000 zimetoka NFRA.