Home | Terms & Conditions | Help

November 24, 2024, 11:51 am

NEWS: WAZIRI MKUU MAJALIWA AMEWAONYA MA DC, RC NA WAKURUGEZI KUFUATA SHERIA

Dodoma: WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amewataka Wakuu wa Wilaya na Wakurugenzi wa Halmashauri nchini kuzingatia mipaka ya madaraka yao na kuhakikisha hatua wanazochukua katika utendaji wao zinafuata Sheria ,Kanuni na Taratibu katika Utumishi wa Umma

Ametoa kauli hiyo jana (Jumanne, Mei 9, 2017) wakati akifungua mafunzo kwa Wakuu wa Wilaya na Wakurugenzi wa Halmashauri za Wilaya katika ukumbi wa Hazina mjini Dodoma. Amesema viongozi hao wanatakiwa kusimamia kikamilifu nidhamu katika Utumishi wa Umma kwa sababu wenyewe ni kioo katika kuishi kwa kuzingatia miiko ya Utumishi wa Umma.

Aidha,Mh. Waziri Mkuu amesema mafunzo hayo yanalenga kuwajengea uwezo na kuendelea kuwaimarisha zaidi katika kusimamia shughuli za Serikali na maendeleo kwenye maeneo yao.

Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu amewataka viongozi hao kutoa kipaumbelea katika kufuatilia na kusimamia kwa makini sekta za afya, kilimo, elimu na maji kwa kuwa ndizo zinazogusa zaidi maisha ya wananchi .

Pia amewaelekeza wasimamie na kuziba mianya yote ya upotevu wa dawa katika vituo vya kutolea huduma za afya na kudhibiti migogoro ya wakulima na wafugaji pamoja na kusimamia usafi na utunzaji wa mazingira katika maeneo yao.