Home | Terms & Conditions | Help

November 24, 2024, 9:59 pm

NEWS: WAZIRI MKUU AWAJIBU ACT WAZALENDO

WAZIRI Mkuu wa Tanzania Kassim Majaliwa amekijibu chama cha ACT Wazalendo Visiwani Zanzibar kuwa ataendelea kutoa maagizo mahala popote nchini kwa kuwa yeye ndiye Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kwamba maagizo aliyoyatoa hivi karibu visiwani humo ni sahihi.

Kauli hiyo ya Waziri Majaliwa imekuja mara baada ya Chama cha ACT Wazalendo upande wa Zanzibar kupitia kwa Mwenyekiti wa Kamati ya Fedha, Nassor Mazrui, kupinga vikali agizo alilolitoa Waziri Mkuu wiki iliyopita katika ziara yake visiwani humo wakati akikagua miradi ya maendeleo.

Bw. Mazrui alisema Waziri Mkuu Kassim Majaliwa hana mamlaka ya kuingilia na kutoa maagizo Zanzibar kwa mambo ya yasiyo ya Muungano kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya 1977 na Katiba ya Zanzibar ya 1984 ambapo alidai zimeainisha waziwazi mamlaka ya Serikali mbili zilizopo.

Hata hivyo jana Majaliwa alitoa alijibu mapigo hayo jijini Dodoma, wakati akifunga semina ya ushiriki wa vyombo vya dola katika usimamizi na udhibiti wa rasilimali madini, ambayo ilihudhuriwa na makamanda wa polisi wa mikoa, wakuu wa vyombo vya usalama, wapelelezi wa mikoa pamoja na watendaji wa Wizara ya Madini.

Waziri Mkuu alisema yeye ndiyo Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania hivyo anapaswa kutoa maagizo mahali popote pale Tanzania Bara au Tanzania Visiwani

“Nimekuja kufunga kikao hichi cha kazi, nitumie fursa kutoa maagizo mbalimbali ndiyo utaratibu wetu lazima tuelezane, lazima tuambizane ili tuweze kufanya kazi vizuri.

“Nakumbuka nilifanya ziara hivi karibuni visiwani, nilikagua miradi na niliona kazi nzuri inafanywa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, nilipokuja kutoa maagizo ikaonekana sipaswi kutoa maagizo mimi Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

“Napaswa kwenda mikoa yote nchini kuona shughuli za miradi zinavyotelezwa lakini mimi pia ndiyo mtendaji mkuu na nimepewa jukumu la kusimamia ilani ya Chama Cha Mapinduzi ambacho kipo katika pande mbili.

“Nipo tayari kutoa taarifa kwenye mkutano mkuu na kwa hiyo nikifika katika mradi nitauona, nitapongeza, nitasikia lakini pale panapokuwa na ubovu nitaeleza, siwezi kuwa naenda nasifia tu hata vile ambavyo vibovu halafu nikarudi nitakuwa sijawatendea haki Watanzania.

“Kwa hiyo nilichokifanya ni sahihi na hasa maeneo ambayo watanzania wanapata tija na Tanzania ni Bara na Visiwani. Na nyie mnapopita huko angalieni haya ambayo yanafanywa na yote yawe na tija kwa watanzania pale ambapo panahitaji marekebisho waambieni,” alisema.

Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu aliwataka wakuu hao wa vyombo vya dola kuhakikisha wanalinda rasilimali za nchi na kuhakikisha zinatumika vyema.

“Ni wajibu wetu kwa pamoja katika nafasi tulizonazo kuhakikisha tunavutia wawekezaji wapya katika maeneo yetu. Hili la kuvutia wawekezaji hususani kwenye sekta ya madini linaweza kuongeza tija kwenye maeneo mbalimbali ya kiuchumi na kijamii ikiwa litasimamiwa vyema,” alisema.