Home | Terms & Conditions | Help

November 26, 2024, 11:40 am

NEWS: WAZIRI MKUU AONYA WATAKAOKWAMISHA SHUGHULI ZA SERIKALI.

DODOMA: WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amezindua mifumo miwili ya kielektroniki itakayosaidia kuandaa bajeti kwenye ngazi ya Serikali za Mitaa

Lengo la Mifumohiyo kuzinduliwa ni Kupanga Mipango, Kuandaa Bajeti ya Kutolea taarifa za hatua za Utekelezaji wa Bajeti (Planning, Budgeting and Reporting System- PlanRep) pamoja na mfumo wa Kufanya Malipo na Kutoa Taarifa za fedha ambazo zimetumwa kwenye Vituo vya Kutoa Huduma (Facility Financial Accounting and Reporting System-FFARS).

Akizindua mifumo hiyo leo mjini Dodoma, Waziri Mkuu amesema lengo la mifumo hiyo mipya ni kuongeza uwajibikaji na ufanisi, na kamwe isiwe kikwazo katika utoaji wa huduma kwa jamii.

“Napenda kutumia fursa hii kuwafahamisha Viongozi na Watendaji pamoja na Wananchi wote kwamba, lengo la matumizi ya mifumo ya TEHAMA ni kuongeza uwazi, uwajibikaji na ufanisi katika utendaji kazi wa shughuli za Serikali na isitumike kukwamisha shughuli au utaratibu wa kazi za Serikali.”

Amesema ni muhimu mifumo hiyo itumike kwa ufasaha ili kuleta tija inayotarajiwa na kila muhusika kwa ahakikishe anailinda, anaitunza na kuitumia mifumo hiyo ili iweze kudumu na kuwa endelevu kwa manufaa ya Taifa.

Pia Waziri Mkuu amewataka viongozi wa mikoa na halmashauri na Vituo vya kutoa huduma za Elimu na Afya kutoa taarifa ya mapato na matumizi kwa mamlaka zinazohusika kwa wakati.

Amesema ngazi zote za Mamlaka za Serikali za Mitaa zitoe taarifa za mapato na matumizi kwa Wananchi wanaowahudumia kupitia mikutano, mbao za matangazo, tovuti, vyombo vya habari na njia nyinginezo.

Waziri Mkuu amesema kwa sasa Serikali haitarajii kuona kituo chochote cha kutoa huduma za Elimu na Afya kilichopo chini ya Halmashauri kinakuwa na matumizi yasiyozingatia taratibu na kanuni za fedha za umma.

“Hatutarajii kuona viongozi wa mikoa na halmashauri wakibadilisha matumizi ya fedha bila kuwasiliana na Mamlaka husika. Matumizi ya fedha yafanyike kutegemea chanzo cha fedha kilichopokelewa kwa wakati na kwa mujibu wa bajeti iliyotengwa kwa mwaka husika.”

Amesema mifumo hiyo imeshirikisha Wizara za Kisekta na Taasisi za Serikali ikiwemo Wakala wa Serikali Mtandao (e-Government Agency-eGA) kuanzia hatua za awali za ukusanyaji wa mahitaji hadi utengenezaji wa mifumo na ndiyo itakayotumika katika Halmashauri na Vituo vya kutolea Huduma za Jamii.

Waziri Mkuu amesema iwapo kuna mdau anataka kushirikiana na Serikali anapaswa kutumia na kuboresha mifumo hiyo na siyo kuleta mifumo mingine kwa sababu uwingi wa mifumo huondoa ufanisi na uwajibikaji.

“Serikali ina matarajio makubwa na mifumo hii, na nitapenda Ofisi ya Rais - TAMISEMI na Ofisi yangu zipate taarifa zote za mipango, bajeti pamoja na taarifa za fedha zinazopelekwa kwenye Mamlaka za Serikali za Mitaa kwa wakati na zikiwa katika ubora wa hali ya juu.”

Kwa upande wake, Kaimu Balozi wa Marekani Nchini Tanzania Bi. Inmi Patterson amesema mifumo hiyo iliyozinduliwa leo itaisaidia Serikali ya Tanzania katika mapambano dhidi ya vitendo vya rushwa na uboreshaji wa huduma za jamii.

Amesema Serikali ya Marekani inaungana na Serikali ya Tanzania katika vita dhidi ya vitendo vya rushwa na ufisadi kwa sababu vinakwamisha utoaji wa huduma mbalimbali za maendeleo kwa jamii.

“Ufisadi ni ugonjwa hatari na unaua kama magonjwa mengine yanavyoua. Ufisadi unazuia maendeleo ya jamii katika nchi husika pamoja na kukwamisha ukuaji wa uchumi na pia unaua ushindani na ndoto za vijana.”

Amesema anatambua namna ambavyo Rais Dkt. John Magufuli na wasaidizi wake wanavyopambana na vitendo vya rushwa na ufisadi ili kuhakikisha fedha zote za maendeleo zinazotolewa zinatumika vizuri.

Naye Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais-Tamisemi George Simbachawene amesema mifumo hiyo itaziwezesha Halmashauri kupunguza gharama kubwa katika kukamilisha zoezi zima la uandaaji wa Mipango na Bajeti kwani zilikuwa zikitumia muda mrefu na gharama kubwa kwenye kuandaa na kuwasilisha Bajeti.

Hesabu za mwaka 2017/2018 zilizotolewa zinaonyesha kuwa gharama za mchakato wa maandalizi ya Mipango ya Bajeti ya mwaka kwa Halmashauri 185 ni takriban sh. Bilioni 8.32 za kulipia usafiri (Mafuta), posho ya kujikimu, shajala na gharama za kudurufu Vitabu.