Home | Terms & Conditions | Help

November 26, 2024, 12:37 am

NEWS: WAZIRI LUGOLA AWAONYA WANAOWARUBUNI WAKIMBIZI NCHINI

WAZIRI wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Kangi Lugola amewaonya baadhi ya watu na taasisi zinazotoa huduma kwa wakimbizi watakao zorotesha kazi ya kuwaondoa wakimbizi nchini Burundi kwa sababu ya kuwarubuni, kupotosha namna Tanzania na Burundi zinavyosimamia.

Alisema taasisi hizo, hutoa kauli za kuwatia woga wakimbizi kwamba Burundi hakuna amani ili wasirudi kwao.

“Yeyote atakayebainika kuhusika na hilo ikiwemo mtu binafsi, mashirika atashughulikiwa ipasavyo,”alisema.

Lugola amepanga kuwarudisha nchini Burundi wakimbizi wote kuanzia Oktoba mosi, mwaka huu.

Akizungumza na waandishi wa habari mkoani Kigoma jana Agosti 25, 2019 Waziri Lugora alisema huo ni msimamo wa Serikali ya Tanzania.

Alisema kuanzia sasa ni wakimbizi wote wa Burundi wanaohifadhiwa kwenye makambi mbalimbali mkoani Kigoma wanaondoka katika kipindi kifupi kijacho na hakuna tena mjadala kuhusiana na jambo hilo.

Alisema katika hilo watatekeleza makubaliano ya pande hizo tatu ambazo ni Serikali ya Tanzania, Burundi na Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi (UNHCR) kurudisha wakimbizi 2,000 kila wiki kwenda Burundi.

Alisema Tanzania na Burundi zimekubaliana kusimamia kazi hiyo hata kama hakutakuwapo msaada wowote kutoka jumuia za kimataifa kusaidia kurudishwa kwao kwa wakimbizi hao.

Alisema sababu kubwa iliyowafanya wakimbizi kukimbia nchi yao, ni kuwapo hali mbaya ya usalama ,lakini sasa hali haipo na wakimbizi hao wanapaswa kurejea.

Alisema Serikali ya Tanzania inatekeleza mikataba ya kimataifa kuhusu kuwapokea, kuwahifadhi na kuwarudisha kwao wakimbizi na haitawalazimisha wakimbizi kurudi kwao, lakini wakati wanaingia nchini sababu ilikuwa kutokuwapo amani.

“Amani imerejea Burundi,sababu hii haitoi nafasi kwa wakimbizi kupata hadhi ya ukimbizi nchini, hilo ni agizo la Serikali,”alisema.