- BREAKING NEWS: TANZANIA YAKANUSHA KUWASHIKILIA KINA DR SLAA NA MWAMBUKUZI
- BREAKING NEWS: RAIS WA MAPINDUZI WA NIGER AMTEUA WAZIRI MKUU MPYA
- BREAKING NEWS: SHILINGI YA KENYA YAPOROMOKA VIBAYA DHIDI YA DOLA
- BREAKING SEREKALI YA RWANDA YAKASIRISHWA NA UBELGIJI KUTOMUIDHINISHA BALOZI WAKE
- BREAKING NEWS: RAIS KIM AKUTANA NA WAZIRI WA ULINZI WA URUSI
NEWS: WAZIRI KALEMANI ALIAGIZA JESHI LA POLISI KUWAKAMATA WAKANDARASI KATAVI
WAZIRI wa Nishati,Nchini Tanzania Dk. Medard Kalemani, ameagiza jeshi la polisi mkoani Katavi kuwakamata mara moja wakandarasi wa Kampuni ya China Railways Construction Electrification Bureau Group Co Ltd (CRCBEG) baada ya kuonekana wakisuasua kusambaza umeme vijijini.
Waziri Kalemani, alimwagiza Kamanda wa Polisi Mkoa wa Katavi, Benjamin Kuzaga kushikilia hati za kusafiria za raia wawili wa China ambao ni wakandarasi wa kampuni hiyo, baada ya kutoridhishwa na kasi yao ya usambazaji na uwashaji umeme vijijini (REA) awamu ya tatu.
Pia aliagiza wakandarasi wote wa kampuni hiyo wanaofanya kazi ya mradi huo, lakini wanaishi Dar es Salaam badala ya Katavi warudi haraka kuendelea na kazi.
Maagizo hayo yalitolewa jana wakati Waziri Kalemani alipohutubia wakazi wa Kijiji cha Sosayati, Manispaa ya Mpanda, baada ya kuzindua na kuwasha umeme.
Alisema hafurahishwi na utendaji kazi wa kampuni hiyo iliyopewa jukumu la kusambaza umeme Mkoa wa Katavi kutokana na kuwa na kasi ndogo ya utekelezaji.
“Nilitoa mwezi mmoja eneo lote la kilometa 27 muwe mmeshawashiwa umeme, lakini mpaka sasa bado, Kijiji cha Majimoto hamjawashiwa, nimepita hapa sijaona vibarua wakihangaika wala nguzo hazijafika, nimefika shule ya sekondari kule nguzo hazijafika na wala hamjasambaza popote,” alisema Dk. Kalemani.
Pia aliwaagiza mameneja wa Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) kutoondoka eneo hilo ili kuhakikisha kazi ya usambazaji umeme inafanyika kwa kasi zaidi.
“Nataka umeme ufike Kijiji cha Majimoto ifikapo Septemba 5, mameneja wote mtabaki hapa kusimamia kazi,” aliagiza.
Akizungumza na wananchi wa Kijiji cha Ntibiri, alisema Serikali imetoa Sh bilioni 89 kwa usambazaji umeme mkoani hapa.