Home | Terms & Conditions | Help

November 25, 2024, 1:54 pm

NEWS: WAZIRI KALEMANI AIOMBA WIZARA KUJENGA CHUO KIKUU CHATO

Chato. Mbunge wa Chato (CCM), na Waziri wa Nishati Dk Merdard Kalemani ameiomba Wizara ya Elimu kujenga chuo kikuu wilayani Chato Mkoa wa Geita ili wanafunzi wanaomaliza elimu ya sekondari waweze kujiunga na chuo hicho.

Ametoa kauli hiyo leo Alhamisi Oktoba 2, 2019 katika hafla ya uwekaji jiwe la msingi katika chuo cha mafunzo ya ufundi cha wilaya ya Chato, akibainisha kuwa tayari wilaya imetenga eneo kwa ajili ya ujenzi wa chuo kikuu.

Akizungumzia chuo cha Veta, Dk Kalemani ambaye ni Waziri wa Nishati ameomba chuo hicho kinachojengwa kwa Sh10.7 bilioni kufundisha lugha za kimataifa ili vijana wa Chato waweze kujifunza na kupata ujuzi wa kuwahudumia watalii watakao tembelea Hifadhi ya Burigi Chato.

Mkuu wa mkoa wa Geita, Robert Gabriel amesema ni muhimu Chato kuwa na chuo kikuu cha afya kwa kuwa hospitali ya kanda inajengwa katika wilaya hiyo, “ni jambo zuri chuo kikajengwa kwa ajili ya wanafunzi wa wa afya.”

Chuo cha wilaya ya Chato kinatarajia kudahili wanafunzi 480 wa muda mrefu na 800 wa muda mfupi na hadi sasa kimekamilika kwa asilimia 78 na kinatarajiwa kukamilika mwishoni mwa Novemba, 2019.