Home | Terms & Conditions | Help

November 26, 2024, 9:15 pm

NEWS: WAZIRI JAFO ASHUSHA NEEMA KWA WANAFUNZI WALIOFAULU KUJIUNGA KIDATO CHA TANO.

DODOMA: Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Selemani Jafo ametoa fursa ya wiki mbili kwa wanafunzi waliofaulu kujiunga na kidato cha tano kufanya mabadiliko ya machanganuo ya tahsusi na kozi mbalimbali walizochagua kwenye fomu ya F4 Selform.


Fursa hiyo inatolewa mwaka huu kwa mara ya kwanza ambapo itawawezesha wanafunzi kurekebisha mchanganuo kulingana na ufaulu waliopata kwenye matokeo ya kidato cha nne mwaka 2018 yaliyotangazwa na Baraza la Mitihani Tanzania(NECTA).

Hayo yameelezwa leo na waziri huyo wakati akizungumza na waandishi wa habari leo ofisini kwake jijini Dodoma amesema wiki hizo mbili zitaanzia Aprili mosi hadi 14 mwaka huu.

Hata hivyo amesema inatokana na baadhi ya wanafunzi walioshindwa kujaza vizuri kwa uhakika tahasusi au kozi zao kutokana na kutokuwa na uhakika wa ufaulu katika masomo yao.

Waziri Jafo amesema ofisi yake imetoa fursa hiyo kwa wahitimu kubadili mchanganuo ili kutoa mwanya zaidi kwa mwanafunzi kusoma fani au tahasusi itakayomwandaa kuwa na utaalam fulani katika maisha yake ya baadae kwa namna ambayo anatamani yeye mwenyewe au kwa kushauri na wazazi au walezi wake.

Amesema ofisi yake imeshakamilisha zoezi la awali la kuingiza taarifa zilizo kwenye Selform za wanafunzi kwenye kanzidata ya TAMISEMI na mabadiliko hayo yatakayofanyika kwa njia ya mtandao yakikamilika kanzidata hiyo ndiyo itakayotumika kuwachagua na kuwapangia kidato cha tano na kozi za vyuo

Waziri Jafo amesema kwa yeyote atakayekuwa hajabadili taarifa zake mpaka muda huo kwisha ofisi yake itaamini kwamba wanafunzi huyo ameridhika na machaguo yake ya tahasusi aliyofanya hapo awali alipokuwa shuleni..