Home | Terms & Conditions | Help

November 26, 2024, 9:21 pm

NEWS: WAZIRI BITEKO WAJUMBE WA GST KUSIMAMIA UBORESHAJI WA HUDUMA ZA MAABARA.

DODOMA: Waziri wa Madini Doto Biteko amewataka wajumbe wa Bodi ya Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania(GST) kusimamia uboreshaji wa huduma za maabara za uchunguzi na upimaji wa miamba na madini yake ili kukidhi viwango vya kimataifa.

Pia amewataka kuweka mikakati thabiti ya kupatikana kwa taarifa za utafiti na uchimbaji wa madini ikiwemo ambazo utafiti wake ulishakwisha.

Biteko ametoa agizo hilo jijii hapa wakati akizindua bodi hiyo, na kusema kuwa serikali ilifanya marekebisho katika sheria ya madini ya mwaka 2010 kwa lengo la kuimarisha usimamizi wa serikali katika sekta ya madini.

“Lengo ni kwamba rasilimali madini tulizojaliwa na mwenyezi Mungu ziwanufaishe watanzania wote, kwa mujibu wa marekebisho hayo ya sheria sambamba na kanuni zake za mwaka 2018, bodi ya GST imeundwa ili kusimamia utekelezaji wa majukumu ya taasisi hiyo,”amesema.

Biteko aliyataja majukumu ya Bodi hiyo kuwa ni kutathimini utendaji kazi wa GST, kupitisha bajeti taasisi, kusimamia utekelezaji wa majukumu ya GST na kuhakikisha GST inajengewa uwezo ili kutekeleza majukumu yake ipasavyo.

Amesema, katika nchi za afrika mashariki Tanzania ndio nchi pekee ambayo ina maabara ya kisasa upimaji wa madini, hivyo lazima wahakikishe wanaitangaza ili nchi nyingine zilete sampuli zao kuja kupima huku na kukuza uchumi.

Waziri huyo alifafanua kuwa taarifa hizo ni muhimu sana kwa nchi na kwa uwekezaji katika sekta ya madini hasa kwa wachimbaji wadogo ambao hawana uelewa mpana wa jiolojia,

Biteko amesema, anaimani kwamba bodi hiyo itatoa ushirikiano mkubwa kwa GST kwa kiasi kikubwa namna ya kupata taarifa hizo na hata zile ambazo utafiti wake ulishaisha.

“Ninatambua miongoni mwenu kuna kamishna wa madini, kamishna wa Tume ya Madini na Katibu Mtendaji wa Tume ya Madini ambako leseni zote za utafiti na uchimbaji wa madini zinatolewa,”amesema.

Amewatahadharisha kuwa, kazi waliyopewa ni kubwa na nyeti sana kwa maendeleo ya sekta ya madini nchini, hivyo wanawajibu wa kutekeleza majukumu ya yaliyoainisha katika bodi hiyo kikamilifu.

Mwenyekiti wa Bodi hiyo Profesa. Justinian Rwezaula, wamepokea maelekezo yote ikiwemo uboreshaji wa huduma za maabara ili ziweze kukidhi viwango vya kimataifa ili kuvutia wawekezaji katika sekta ya madini kutumia zaidi maabara za hapa nchini badala ya kupeleke sampuli katika maabara za nje.