Home | Terms & Conditions | Help

November 27, 2024, 3:37 am

NEWS: WAZIRI AINYANG'ANYA MANISPAA YA ILALA SH. BILIONI 3

Dar es Salaam: Naibu waziri wa fedha na Mipango, Dk Ashatu Kijaji ameinyang'anya Manispaa ya Ilala, Jijini Dar es Salaam Sh3 bilioni ilizoipatia kwa ajili ya kutekeleza mradi wa kimkakati wa machinjio ya kisasa ya Vingunguti. Uamuzi huo umetokana na manispaa hiyo kushindwa kutekeleza kwa wakati mradi huo wenye thamani ya zaidi ya Sh8.5bilioni.

Dk Kijaji ametoa Uwamuzi huo leo Februari 19, 2019 mara baada ya kutembelea na kukagua maendeleo ya mradi huo.

Amesema Serikali ilitoa Sh3 bilioni kati ya Sh8.5 bilioni kukamilisha mradi wa machinjio ya Vingunguti kuanzia Mei, 2018, lakini hadi sasa fedha hizo hazijatumika. “Fedha haziwezi kukaa kwa mwaka mzima bila matumizi ilihali kuna maeneo mengine ambako fedha hizo zinahitajika kwa ajili ya utekelezaji wa miradi, hivyo tunazichukua fedha hizi na Manispaa ya Ilala mtalazimika kuomba upya mtakapokuwa mmejipanga," alieleza Dk Kijaji.

Dk. Kijaji amefafanua kuwa taratibu za fedha za Serikali zinazopelekwa kwenye miradi zinatakiwa zianze kutumika ndani ya miezi mitatu lakini Manispaa ya Ilala haijazitumia fedha hizo huku karibu Mwaka wa Fedha ukikaribia kumalizika. "Tunaiangusha dhamira njema ya Mheshimiwa Rais Dk John Pombe Magufuli ya kuwahudumia Watanzania waliosubiri kuhudumiwa, ndio maana tukaanzisha miradi hii ya kimkakati ya kuongeza mapato ya halmashauri na mkaleta maandiko yenu Serikali ikatoa fedha kumbe hamko tayari na mnatukwamisha kutekeleza Ilani ya Chama cha Mapinduzi," alisema.

"Tumewapatia fedha mmeshindwa, kwa hiyo wana Ilala na wana Vingunguti, kwamba Serikali yao ina dhamira njema lakini wapo wanaotuangusha hivyo tutazichukua fedha hizi mpaka hapo Manispaa ya Ilala watakapoleta mpango kazi unaotekelezeka na si huu ambao hawakujiandaa," alisisitiza.