Home | Terms & Conditions | Help

November 26, 2024, 11:25 am

NEWS: WANAWAKE 3 WAFARIKI DUNIA WAKIENDA KUJIFUNGUA

MOROGORO: Ukosefu wa zahanati na ubovu wa miundombinu katika Kata ya Mabula wilayani Kilosa mkoani Morogoro, imesababisha wanawake watatu kupoteza maisha wakati wakiwahishwa kujifungua katika hospitali ya Berega katika kipindi cha mwaka 2015/16.

Wakizungumzia changamoto hizo, wanawake hao akiwamo Wema Matowe, mkazi wa Kijiji cha Magera Kata ya Mabula alisema kituo cha afya kilichopo ya Mabula hakina uwezo wa kuwasaidia kinamama kujifungua kwa upasuaji bali wa njia ya kawaida.

Alisema ukosefu wa huduma za upasuaji umesababisha vifo hivyo na hali hiyo inaendelea kuwatia wasiwasi wanawake wa kijiji hicho na kata nzima.
“Nimeshuhudia kwa macho yangu kinamama watatu wakifa miaka ya hivi karibuni, tunapata wasiwasi, lakini hali ya uchumi kwetu ndio tatizo, tunaweza kukusanya matofali na kujenga zahanati, ila hatuwezi kukamilisha ujenzi,” alisema Matowe.

Alimwomba Mbunge wa Jimbo la Kilosa Mashariki kuona umuhimu wa kutekeleza ahadi zake kwa kuwasaidia ujenzi wa zahanati.

Naye Hadija Bakari aliiomba Serikali kuangalia namna ya kuboresha huduma za kinamama wajawazito katika zahanati ya kijiji hicho, kwani huduma zilizopo katika zahanati ya Kata ya Mabula hazikidhi mahitaji kufuatia kuwa na kipimo kimoja tu cha kuangalia upungufu wa kinga mwilini.

“Ukifika utapimwa tu mimba na Ukimwi, lakini hakuna huduma ya kipimo cha wingi wa damu, makundi ya damu na shinikizo la damu, magonjwa ambayo humpata au huhisiwa kumpata mjamzito mara nyingi na mtu kutakiwa kwenda hospitali ya Berega ambako ni mbali,” alisema.

Diwani wa Mabula, Meshack Chalo, alikiri kutokea kwa vifo hivyo katika kata hiyo na changamoto ya barabara imesababisha kwa kiasi kikubwa wajawazito kupoteza maisha kufuatia kulazimika kupita njia ndefu ya urefu wa kilomita 25 badala ya kilomita saba ambayo ina eneo korofi la daraja ambalo linatakiwa kujengwa, ili kupitika kwa urahisi na kufika Hospitali ya Berega pale inapohitajika.