Home | Terms & Conditions | Help

November 25, 2024, 9:41 am

NEWS: WANAHARAKATI WA JINSIA MOJA WAILAUMU UGANDA

Wanaharakati wanaotetea haki za watu wa jinsia moja nchini Uganda wanalaani kitendo cha polisi wa nchi hiyo kuendelea kuwashikilia watu waliokamatwa mwishoni mwa wiki hii iliyopita jijini Kampala kwa madai ya kujihusisha na mapenzi ya jinsi moja.

Jumapili usiku polisi jijini Kampala, waliwakamata zaidi ya watu 120 wanaodaiwa kujihusisha na mapenzi ya jinsia moja waliokuwa katika eneo moja ya burudani katika barabara ya Hanington.

Frank Mugisha, mwanaharakati maarufu wa haki za watu wa mapenzi wa jinsia moja, anadai kuwa watu wengi walikamatwa kwenye baa hiyo inayoruhusu watu wa mapenzi ya jinsia moja ,hali inayoashiria vitisho dhidi ya watu wa jamii hiyo.

Lakini msemaji wa jeshi la polisi mjini Kampala amekana kuwa walikuwa kwenye operesheni dhidi ya watu wanaojihusisha na mapenzi ya jinsia moja.

Polisi wamesema walipewa taarifa na raia wema kuwa dawa za kulevya zilikua zikivutwa kwenye baa hiyo. Kisha wakaamua kufanya uvamizi wakati wa usiku.

Nchini Uganda sheria inaelezea kitendo cha ngono kinyume na maumbile kama mwanamume kushiriki ngono na mwanamume mwengine au mwanamke kwa mwanamke.

Miezi kadhaa iliyopita waziri wa maadili nchini Uganda alisema kuwa shughuli zote za wapenzi wa jinsia moja ni haramu na kinyume na tamaduni za watu wa Uganda.