Home | Terms & Conditions | Help

November 24, 2024, 5:59 pm

NEWS: WANAFUNZI 5 WAPOTEZA MAISHA BAADA YA KUGONGWA NA GARI RUVUMA

Wanafunzi watano wa shule ya msingi Ndelenyuma katika halmashauri ya wilaya ya Madaba wilayani Songea mkoani Ruvuma wamefariki dunia na mmoja kujeruhiwa baada ya kugongwa na gari aina ya Toyota Land Cruiser la kampuni ya Kamsat.

Akizungumza kwa niaba ya Kamanda wa polisi wa mkoa wa Ruvuma Kamishna Msaidizi wa polisi Pili Mande amesema wanafunzi hao walikufa hapo hapo baada ya kugongwa na gari hilo.

Miili miwili kati ya mitano ilikutwa barabarani huku miili mitatu ikisombwa na maji hadi mita mia moja na kutupwa korongoni kutokana na mvua kubwa iliyonyesha na mmoja akijeruhiwa.

Kamanda Mande amesema wanaendelea na uchunguzi na mara tu watakapokamisha, hatua za kisheria zingine zitafuata.

Akiongea leo Februari 12, 2020 na Waandishi wa Habari Kamanda wa Polisi mkoani Ruvuma, Simon Maigwa amesema wanafunzi hao ni Glory Kilasi (12) alikuwa akisoma darasa la nne, Ushindi Juma (12) darasa la nne, Evaristo Miligo (10) darasa la pili, Isaya Mkani (13) darasa la nne na Victor Luoga (10) darasa la kwanza.

“Majeruhi ni Hilda Kilasa (12) mwanafunzi wa darasa la nne ambaye alitibiwa na kuruhusiwa na hali yake inaendelea kuimarika” amesema Maigwa

Maigwa amesema gari lililowagonga wanafunzi hao ni mali ya kampuni ya Camusat lililokuwa linatokea Songea kwenda Madaba liliendeshwa na dereva aliyefahamika kwa jina moja la Salum.