Home | Terms & Conditions | Help

November 25, 2024, 11:03 am

NEWS: WAMACHINGA NEEMA YAWASHUKIA

MWANZA: RAIS John Magufuli ametua jijini Mwanza jana na kufunika kwa mapokezi makubwa huku akisema kwamba kamwe hatakubali kuwaona wafanyabiashara wadogo nchini maarufu kama wamachinga wakisumbuliwa na kushindwa kufanya biashara.

Aidha, amesema atahakikisha kuwa dhuluma zilikuwa zinafanywa kwa wananchi wanyonge haziwezi kupata nafasi kwenye serikali yake. Rais Magufuli aliyasema hayo muda mfupi wakati alipowahutubia mamia ya wakazi wa Mwanza waliojitokeza kwa wingi katikati ya Jiji la Mwanza kumlaki baada ya kuwasili jijini hapa kwa ziara ya kikazi ya siku mbili.

Kabla ya kutoa hotuba yake katikati ya Jiji la Mwanza akielekea Ikulu Ndogo ya Mwanza, Rais aliwapungia mkono na kuwashukuru wakazi hao kwa mapokezi makubwa waliyoyaonesha kwake.

Alisema ndani ya uongozi wake atahakikisha wananchi wa kati, wa juu na wanyonge wananufaika na rasilimali za nchi, huku akiwataka Watanzania waendelee kuwa wamoja. “Narudia hakuna machinga atakayesumbuliwa katika nchi hii, na ndio kupitia Bunge tayari imetungwa sheria itakayowawezesha wamachinga kupatiwa vitambulisho,” alifafanua na kuwataka Watanzania popote walipo nchini waendelee kushikamana kwa kufanya kazi kwa pamoja kwa lengo la kujiletea maendeleo na maisha bora.

Rais aliwasili kwenye Uwanja wa Ndege wa Mwanza saa 10.21 jioni na kupokelewa na Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, John Mongella, Waziri wa Maji na Umwagiliaji, Gerson Lwenje, Katibu Mkuu wa wizara hiyo, Profesa Kitila Mkumbo, viongozi wa madhehebu ya dini na mamia ya wananchi wa Jiji la Mwanza waliojipanga barabarani kutoka uwanja huo hadi Ikulu wakimpungia mikono na vigelele vya furaha, huku baadhi yao wakisikika kumtakia afya na maisha marefu.

Leo Rais anaendelea na ziara yake ya kikazi wilayani Sengerema ambako atazindua rasmi mradi mkubwa wa maji wa Nyamazugo uliojengwa kwa gharama ya Sh bilioni 20 ambao unatarajia kutoa huduma ya maji safi na salama kwa wakazi 138,000 na kuwaondolea tatizo la maji la muda mrefu.