Home | Terms & Conditions | Help

November 24, 2024, 2:19 pm

NEWS: WALIOBEBA MIMBA WATAKIWA KURUDI SHULE.

DODOMA: Bunge limeishauri serikali kutoa tamko rasmi mwongozo wa kuwarudisha shuleni wanafunzi wanaopata ujauzito mara baada ya kujifungua.


Ushauri huo ulitolewa bungeni mjini hapa jana na Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii ilipokuwa ikiwasilisha taarifa yake kuhusu utekelezaji wa bajeti ya Wizara ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi mwaka huu wa fedha na mkadirio ya bajeti ya wizara hiyo kwa mwaka ujao wa fedha.


Mjumbe wa kamati hiyo, Hussein Bashe mbunge wa Nzega (CCM), akiwasilisha taarifa kwa niaba ya Mwenyekiti Peter Serukamba, alishauri serikali itoa tamko hilo ili kulisaidia taifa kunufaika na usomeshaji wa watoto wa kike.


Huku akiibua shangwe, nderemo na vifijo miongoni mwa wabunge wanawake, Bashe alisema kamati yake inatambua serikali imeandaa mwongozo huo ambao bado upo kwa wadau kwa ajili ya kupata maoni kabla ya kufanya uamuzi.


"Kamati inashauri serikali kutoa tamko rasmi kwamba mwongozo huo uanze kutumika ili wanafunzi wa kike wanaofukuzwa shule kutokana na kupata ujauzito kurudishwa shuleni ili kuendelea na masomo yao," alisema.


"Mwanafalsafa wa Masuala ya Elimu nchini Ghana, Dk. James Aggrey, aliwahi kusema: Ukimuelimisha mwanaume, umeelimisha mtu mmoja, lakini ukimuelimisha mwanamke, umeelimisha familia nzima".


TRIL.1.6/- ZA MADENI


Wakati Waziri wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufunzi, Prof. Joyce Ndalichako, aliliambia Bunge jana kuwa amelipa Sh. bilioni 10.5 za deni la walimu lililohakikiwa mwaka huu wa fedha, kamati hiyo iliishauri serikali kuharakisha malipo uhakiki wa madeni ya watumishi hao yanayofikia Sh. trilioni 1.6.


NGUVU YA TCU
Bashe alisema kamati hiyo inaunga mkono uamuzi wa Rais John Magufuli alioutoa Aprili 15 wa kuitaka Tume ya Vyuo Vikuu (TCU) iache kuwachagulia wanafunzi vyuo vya kwenda kusoma badala yake iwaache wachague wenyewe.


"Kamati inaona kwa kuwapa uhuru wanafunzi wachague vyuo wanavyotaka kutasaidia serikali kuwalipia ada wanafunzi walioko katika vyuo vya serikali na hatimaye kuupunguza mzigo kwani ada za vyuo vya serikali zinaratibiwa na serikali tofauti na vyuo binafsi," alisema.


Kamati hiyo pia ilishauri serikali iwekeze kwa kiasi kikubwa kwenye vyuo vya ufundi nchini kwa kupitia upya mitaala ya vyuo vya ufundi ili kuhakikisha vinatoa mafunzo yanayoendana na uchumi wa kisasa na viwanda.


Kuhusu uratibu wa shule binafsi, kamati hiyo iliishauri serikali kuhakikisha shule hizo zinatoa taarifa za uratibu huo kwa mzazi kabla hajafanya uamuzi wa kumpeleka mtoto wake katika shule husika ili kupunguza malalamiko ya wazazi.