Home | Terms & Conditions | Help

November 26, 2024, 3:58 am

NEWS: WALIMU 15 DOM WATIMULIWA KAZINI KWA UTORO.

DODOMA: TUME ya Utumishi ya walimu(TSC)wilaya ya Chamwino mkoani Dodoma imewafukuza kazi jumla ya walimu 15 ambapo kati yao walimu 14 wamefukuzwa kutokana na utoro na mmoja kutokana na kukutwa na vyeti feki.


Uamuzi huo umetangazwa leo wilayani humo na Kaimu Katibu Msaidizi wa Tume hiyo KHALID SHABAN, amesema kati ya walimu hao 15 waliofukuzwa nane ni wa shule za msingi na saba ni wa shule za sekondari huku mmoja wa walimu hao akiwa hajaonekana kazini kwa siku 500.


SHABAN amesema walimu hao ambao hakuwataja majina wamekuwa watoro kwa siku 400 na mwingine siku 500 na kusema wamekuwa wakipokea vitisho kutoka kwa viongozi wao lakini wao wamechukua hatua hiyo kwa maslahi ya watoto wanyonge ambao ndio waathirika wakuu.

Aidha ameahidi kuwa kupitia Tume hiyo atahakikisha haki inatendeka kwa walimu watovu wa nidhamu ikiwemo watoro kwa kuwa wapo ambao wamekuwa watoro katika shule za umma lakini anafundisha katika shule binafsi na hivyo kuendelea kupokea mishahara sehemu mbili.

Hata hivyo amesema TSC inataka kujenga misingi imara ya kuhakikisha kunakuwa na kiwango kizuri cha ufaulu katika shule za mkoa wa Dodoma kutokana na mkoa huo kwa muda mrefu kushika nafasi za chini kwenye mitihani ya kitaifa na kuwataka walimu kufuata sheria na taratibu walizojiwekea ili kuendana na kasi ya Rais JOHN MAGUFULI.

Kwa upande wake Mkuu wa Shule ya sekondari ya Buigiri CATHERINE CHILONGANI na mwalimu mkuu wa shule ya msingi ya Chamwino AISHA KIMOLA wamesema hatua zilizochukuliwa kwa walimu hao ambao hawaheshimu kanuni za utumishi wa umma zitasaidia kupandisha kiwango cha ufaulu ambacho kipo chini.