Home | Terms & Conditions | Help

November 25, 2024, 1:49 pm

NEWS: WAKUU WA WILAYA WATAKIWA KUWA MAKINI NA MATAPELI

DODOMA:WAKUU wa Wilaya zote nchini pamoja na Wakurugenzi wa Halmashauri mbalimbali nchini wametakiwa kuwa makini juu ya vitendo vya kitapeli ambavyo vinafanywa na watu wenye nia ovu ambao wamekuwa wakiwapigia simu wakuu wa Wilaya na Wakurugenzi kwa kutumia majina ya mawaziri, manaibu waziri pamoja na makatibu wakuu wa Wizara mbalimbali kuwatapeLi viongozi hao.

Tahadhari hiyo imetolewa leo Mjini Dodoma na Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais-TAMISEMI,Selemani Jafo, wakati alipokuwa akifunga mafunzo ya wakuu wa Wilaya na Wakurugenzi wa halmashauri sita za Mikoa ya Kanda ya Ziwa ambayo yamefadhiliwa na Taasisi ya Uongozi.

Akifunga mafunzo hayo JAFO amesema kwa sasa umezuka utapeli ambao unafanywa na watu wenye nia ovu ambao wanatumia majina ya Mawaziri,Manaibu Waziri,Waziri Mkuu na makatibu wa Wizara mbalimbali kwa kuwatapeli wakuu wa wilaya na wakurugenzi jambo ambalo linawafanya wakuu wa Mikoa,wakuu wa Wilaya na wakurugenzi kutapeliwa.

Amesema matapeli hao wamekuwa wakitumia majina ya viongozi wa ngazi za juu serikalini kwa madai kuwa wanauguliwa au wamepata shida mbalimbali wawapo safarini jambo ambalo siyo kweli.

Katika hatua nyingine Jafo amewataka wakurugenzi pamoja na wakuu wa Wilaya,kufanya kazi kwa misingi ya manufaa mapana kwa jamii na siyo kufanya kazi kwa manufaa yao.

Aidha amesema mafunzo ambayo ni ya siku tano waliyopatiwa na taasisi ya uongozi iwe chachu ya kuwafanya wakuu hao wa wilaya na wakurugenzi kufanya kazi kwa ueledi mkubwa zaidi ,tofauti na ilivyo kuwa hapo awali.

Mbali na hilo Jafo amewataka viongozi hao kuhakikisha wanajikita zaidi katika mambo muhimu kama vile,Afya,Elimu,maji na kilimo.

Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi Taasisi ya Uongozi,DENIS RWEYEMAMU,amesema mafunzo ambayo yanatolewa kwa wakuu wa Wilaya na wakurugenzi ni ya kuwajengea uwezo ili kuweza kufanya kazi kwa malengo ya maendeleo.


Aidha Mafunzo hayo yametolewa kwa Wakuu wa Wilaya na wakurugenzi wa Halmashauri za kanda ya ziwa ambapo ni Mikoa ya Mara,Mwanza,Kagera,Simiyu, na Geita lengo kuwajengea uwezo katika muingiliano wa ksiasa na kiutawala,muundo na majukumu ya utawala za mikoa na Serikali za Mitaa,sekretarieti za mikoa udhibiti wa madawa ya kulevya.