Home | Terms & Conditions | Help

November 26, 2024, 10:00 am

NEWS: WAKULIMA WAKABILIWA NA CHANGAMOTO YA UKOSEFU WA MIUNDOMBINU YA USAFIRISHAJI WA MAZAO

DODOMA: IMEELEZWA kuwa wakulima wengi nchini wanakabiliwa na changamoto kubwa ya ukosefu wa miundombinu ya uhakika ya usafirishaji mazao kutoka maeneo ya vijijini hadi kufika eneo la kuuzia mazao hayo.

Akizungumza leo na wadau wa Programu ya Miundombinu ya Masoko, Uongezaji Thamani na Huduma za Kifedha vijijini (MIVARF) Mkurugenzi Idara ya uratibu shughuli za serikali ofisi ya waziri mkuu Obey Assey amesema kuna kila sababu ya kuhakikisha kuwa kunakuwa miundombinu rafiki katika sekta ya kilimo.

Mpango huo kitaifa wa miaka 7 ulionza mwaka 2011 unataraji kufikia ukomo mwaka 2018 ambapo lengo kuu ni kupunguza umaskini wa kipato na kuimarisha uhakika wa chakula kwa njia endelevu kwa wazalishaji wadogo vijijini ambao wanakabiliwa na changamoto ya ubovu wa miundombinu ikiwemo barabara.

Assey amesema kuna umuhimu mkubwa wa kuboresha masoko katika sekta ya kilimo ili kuongeza dhamani na hatimaye kukuza uzalishaji wa mtu mmoja mmoja na hatimaye kukuza pato la taifa.

Walter Swai ni mratibu wa mpango huo amesema kupitia program hiyo wamelenga kumuwezesha mkulima kuwa na mazingira wezeshi ya kufanya biashara.

Juma Mene Mkulima Singida na Davis Temba Mkulima Arusha ni baadhi ya wakulima ambao ni wanufaika kutoka maeneo mbalimbali nchini wamesema kupitia mpango huo umewezesha kuongeza thamani ya uzalishaji na hatimaye kukabiliana na changamoto ya masoko.

Mpango wa uboreshaji wa miundombinu ya masoko,uongezaji dhamani na huduma za kifedha vijijini MIVARF unatekelezwa Tanzania Bara na visiwani kwenye mikoa 29 na Halmashauri 73 nchini.