Home | Terms & Conditions | Help

November 26, 2024, 6:37 am

NEWS: WAKIMBIZI MBARONI KISA FUJO KAMBINI

KIGOMA: JESHI la polisi Mkoa wa Kigoma, linawashikilia wakimbizi 19 wa Kambi ya Nduta iliyopo Wilaya ya Kibondo kwa tuhuma za kufanya fujo.


Kamanda wa polisi Mkoa wa Kigoma, Ferdinand Mtui, alisema vurugu hizo zilidumu kwa takribani saa sita kambini hapo jana.

Kamanda Mtui alisema wakimbizi hao walifanya fujo wakitaka kuvamia na kuvunja ghala la chakula la Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Chakula (WFP).


Alisema wakimbizi hao waliziba barabara kisha kuharibu miundombinu mbali mbali ya shirika hilo wakiwa na lengo la kuchukua chakula kutoka ghalani wakidai kuwa chakula walichopewa ni kidogo na hakitoshi.

Kwa mujibu wa Kamanda Mtui, kufuatia vurugu hizo askari walijipanga vyema kwa kuimarisha ulinzi ikiwamo kufanya doria katika kambi hiyo na kufanikiwa kuwadhibiti.

Alifafanua kuwa ni askari wake pia walifanikiwa kuwakamata wakimbizi 19 ambao wanatuhumiwa kuwa chanzo cha fujo hizo.

Kamanda Mtui alisema upelelezi wa tukio hilo unaendelea ili kuwabaini watuhumiwa wengine waliohusika na tukio hilo pamoja na kutathmini thamani ya miundombini ya shirika hilo ambayo imeharibika.

Kamanda Mtui alibainisha zaidi kuwa watuhumiwa hao watafikishwa mahakamani ili sheria ichukue mkondo wake baada ya uchunguzi kukamilika.