Home | Terms & Conditions | Help

November 25, 2024, 2:34 am

NEWS: WAITARA ATISHIA KUMNG'OA JOHN HECHE JIMBO LA TARIME VIJIJINI

Dar es Salaam. Naibu Waziri Ofisi ya Rais Tamisemi na Mbunge wa Ukonga (CCM), Mwita Waitara ametangaza kumng'oa Mbunge wa Sasa wa Tarime Vijijini John Heche katika uchaguzi mkuu 2020, katika Jimbo hilo mkoani Mara.

Waitara amesema ametangaza kuwa atagombea Ubunge katika Jimbo la Tarime vijijini ikiwa ni ishara kwamba hatogombea tena Ukonga kama alivyofanya mwaka 2015 akiwa Chadema kabla ya kujiuzulu na kutimkia CCM mwaka 2018 alikopitisha kutetea nafasi hiyo na akashinda.

Waitara amesema ametia nia ya kugombea ubunge katika jimbo hilo na atafurahia endapo Chadema itampitisha tena Heche kugombea ili aweze kuchuana naye.

Naibu waziri huyo ametangaza nia hiyo wakati akisherehekea sikukuu ya mwaka mpya na wakazi wa Tarime vijijini sehemu ambayo wazazi wake wanaishi.

“Naiomba Chadema imlete John Heche hapa Tarime Vijijini tukutane, nimesikia anataka kwenda mjini asiende,” alisema Waitara

Alisema kwa mara ya kwanza aligombea jimbo hilo mwaka 2010 akiwa CCM lakini kutokana yeye kuwa masikini alikosa fursa hiyo.

“Wakati huo utaratibu wao ulikuwa mwenye pesa ndiye hupewa nafasi, sikuwa na pesa wala mdhamini ina maana katika familia hii niliingia katika siasa peka yangu, sina shangazi, sina mjomba mimi ni jeshi la mtu mmoja, katika mazingira hayo yaliyotokea yalinifanya mimi kuhama chama wakati ule,” alisema Waitara

Alisema mwaka 2010 alirudi katika jimbo hilo na kuomba ubunge, kazi ikafanyika lakini haikuwezekana, labda Mungu hakupenda jambo ambalo lilimfanya kwenda kuwa mwenyekiti wa mtaa wa Kivule katika jimbo la Ukonga jijini Dar es Salaam.

“Mwaka 2015 nikagombea ubunge kupitia Chadema katika jimbo la Ukonga nikashinda lakini sasa nataka kurudi nyumbani,” alisema Waitara