- BREAKING NEWS: TANZANIA YAKANUSHA KUWASHIKILIA KINA DR SLAA NA MWAMBUKUZI
- BREAKING NEWS: RAIS WA MAPINDUZI WA NIGER AMTEUA WAZIRI MKUU MPYA
- BREAKING NEWS: SHILINGI YA KENYA YAPOROMOKA VIBAYA DHIDI YA DOLA
- BREAKING SEREKALI YA RWANDA YAKASIRISHWA NA UBELGIJI KUTOMUIDHINISHA BALOZI WAKE
- BREAKING NEWS: RAIS KIM AKUTANA NA WAZIRI WA ULINZI WA URUSI
NEWS: WAFUGAJI WAANGULIA KILIO MBELE YA WAZIRI MPINA .
MANYARA; Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Luhaga Mpina amesitisha operesheni ya kuwaondoa na kuwachomea nyumba, mazizi ya mifugo, makambi ya uvuvi Wananchi wa Kijiji cha Vilima vitatu Wilaya ya Babati Mkoa wa Manyara na kuunda timu ya wataalamu kutoka Wizara 8 kufuatilia utekelezaji wa operesheni hiyo na kuwasilisha ripoti hiyo serikalini kwa maamuzi zaidi.
Operesheni hiyo iliyofanyika mwezi Julai mwaka huu imesababisha wananchi wengi kukosa mahali pa kuishi kutokana na nyumba zao kuchomwa moto ambapo sasa wanaishi chini ya miti hali iliyosababisha adha kubwa kwa wanawake wajawazito, watoto na wagonjwa.
Pia mifugo yao kuvamiwa na wanyama wakali na mingine kupotea baada ya mazizi kuchomwa moto, shughuli za uvuvi kusimama baada ya makambi na zana za uvuvi kuteketezwa kwa moto hali ambayo imeleta taharuki kubwa kwa wananchi na kushindwa kujua la kufanya.
Wakizungumza kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika katika Kijiji cha Vilimavitatu na kuhudhuriwa na Mkuu wa Wilaya ya Babati, Elizabeth Kitundu huku idadi kubwa ya wananchi wakiangua vilio mbele ya Waziri Mpina wakionesha masikitiko yao kuhusiana na unyama waliofanyiwa na Serikali ya wilaya hiyo na kumuomba kuwasaidia ili waweze kurudi katika maisha yao ya awali.
Walisema mbali na madhara hayo pia akiba ya chakula walichokuwa nacho majumbani mwao nacho kimechomwa moto hivyo kukosa kabisa chakula na kumuomba afikishe kilio hicho kwa Rais Dk. John Pombe Magufuli ili wapatiwe msaada wa haraka chakula ili kunusuru wasife kwa njaa katika kipindi hiki kigumu wanachopitia.
Waziri Mpina alihoji iweje operesheni hiyo ifanyike huku kukiwa na katazo la Rais Dk. John Pombe Magufuli la Januari 15 mwaka huu la kusitisha operesheni zote za kuwaondoa wananchi wanaoishi kwenye maeneo yanayodaiwa kuwa ni hifadhi hadi hapo itakapoamuliwa vinginevyo.
Waziri Mpina pia ahoji iweje operesheni hiyo ifanyike kwenye eneo hilo huku kukiwa na Hukumu ya Mahakama iliyoliondoa eneo la Kijiji cha Vilima Vitatu kwenye Jumuiya ya Hifadhi ya Wanyapori Burunge (Juhibu) ambapo hukumu hiyo haikukatiwa rufaa wala kutenguliwa na Mahakama.
Pia Waziri Mpina alihoji iweje operesheni hiyo ya kuondoa mifugo ifanyike bila kushirikisha Wizara ya Mifugo na Uvuvi kama Sheria, Kanuni na miongozo inavyoelekeza hali iliyosababisha mifugo mingi kuteseka kwa kukosa huduma muhimu zikiwemo chanjo, dawa, maji na malisho na kusababisha mifugo kupotea na mingine kufa na kusababisha hasara kubwa kwa wafugaji taifa.