Home | Terms & Conditions | Help

November 24, 2024, 11:55 am

NEWS: WABUNGE: WAANDISHI WAPEWE ULINZI MKALI

Dodoma: WABUNGE wameomba serikali iwape ulinzi waandishi kutokana na kuvamiwa na kushambuliwa wanapokuwa katika kuripoti matukio mbalimbali. Wabunge walitoa kauli hiyo bungeni jana wakati wakijadili bajeti ya Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo iliyowasilishwa bungeni Ijumaa iliyopita.


Mbunge wa Temeke, Abdallah Mtolea alisema waandishi wamekuwa hatarini kutokana na ukweli kwamba wamekuwa wakivamiwa wakiwa kazini. Alitoa mfano wa waandishi walivyovamiwa katika studio ya Clauds TV na katika mkutano wa CUF uliofanyika Mabibo, Dar es Salaam, alisema serikali inatakiwa kutoa msisitizo badala ya sasa ambapo kama haioni madhara makubwa kwa waandishi.


Alisema kitendo cha waandishi kudhurika wanapokuwa katika shughuli zao za kuripoti matukio wakitumia weledi wao, serikali inatakiwa kutoa msisitizo wa kuwalinda wana taaluma hiyo. Mbunge wa Viti Maalum, Aida Khenani (Chadema), alisema, waandishi wa habari wanafanya kazi katika hofu, kutokana na kukosa ulinzi, serikali inatakiwa kufanya jitihada kuwalinda waandishi ambao wamekuwa wakivamiwa katika kazi zao. Mbunge wa Ubungo, Saed Kubenea (Chadema) alisema, vyeti vinatakiwa katika kuendeleza taaluma ya uandishi lakini pia taaluma nyingine inatakiwa katika kuboresha kazi za uandishi.

“Vyeti pekee havikufanyi mtu uwe mahiri bali weledi na uadilifu na kufuata misingi ya taaluma kama inavyotastahili. Kubenea alisema mafanikio yanayopatikana kwenye vyombo vya habari hayatokani na waandishi hao kuwa na vyeti tu bali pia taaluma nyingine mbalimbali. Mbunge wa Makete, Profesa Norman Sigalla (CCM) alisema wakati mwingine vyeti peke yake si kipimo halisi ya kubaini utendaji wa mtu, bali ni pamoja na weledi wake.


Alisema hayo kutokana na timu ya taifa kupewa wageni kutokana na kuwa na vyeti vikubwa, lakini wapo wazawa ambao hawana vyeti vikubwa lakini wanafanya kazi vizuri. Mbunge wa Mikumi, Joseph Haule (Chadema) alisema, serikali inatakiwa kuwathamini wasanii na kuwalinda kutokana na mtindo wa sasa ambapo wamekuwa wakitekwa au kuingizwa kwenye matatizo ya wanasiasa.

Haule alisema wasanii wamekuwa wakifanya kazi kwa hofu, wakiogopa kutoa mawazo ya kupitia nyimbo, wakiogopa kutunga nyimbo kutokana na kwamba wanaweza kutekwa au kukamatwa. Alisema wamekuwa wakifanya kazi katika mazingira ya kimasikini na wanatumika kama vyombo ambavyo havija thamani, inatakiwa kuthaminiwa. “Muziki unachangia pato la serikali kwa asilimia moja, inatakiwa kuwekeza kwa wasanii ili wachangie zaidi kwa kuongeza bajketi ya sekta ya sanaa,” alisema.

Wasanii wa filamu wamekuwa wakinyonywa na wakishindwa kutekeleza vizuri majukumu yao kutokana na kutozwa kodi nyingi zikiwamo za bodi, kurekodi, kutozwa kwa nakala na kukagua na mhindi anayesambaza. Wasanii wamekuwa wakivamiwa wanapofanya maonesho yao, hasa TRA wakidai asilimia 18, wizara inatakiwa kuzungumza na mamlaka hiyo kuhusu utaratibu huo ambao unawaumiza wasanii. Mbunge wa Mpwapwa, George Lubereje (CCM) alisema waandishi wengi wanaandika habari za mikoani au mijini na hawaandiki habari za vijijini.