Home | Terms & Conditions | Help

November 24, 2024, 9:22 am

NEWS: WABUNGE NA WATUMISHI 17 WAAMBUKIZWA CORONA KENYA

Ripoti ya hivi karibuni imeonesha kuwa wabunge na wahudumu 17 wameambukizwa virusi vya corona, hali ambayo imezusha wasiwasi kwa wabunge hao.

Zipo taarifa zinasema kuwa, Wizara ya Afya iliwafahamisha maspika kusitisha vikao maalum.

Vikao hivyo maalum vilivyokuwa vifanyike Jumatano vimeahirishwa kwa hofu ya maambukizi miongoni mwa wajumbe wengine.

Zaidi ya wajumbe 200 ambao wamepimwa virusi vya Corona, wakiwemo maspika wa bunge la seneti na la taifa wanaendelea kupokea matokeo ya vipimo vyao kutoka kwa Wizara ya Afya. Kikao maalum cha mabunge hayo kilisitishwa ghafla na maspika ambao wamekanusha madai ya kuwa wajumbe ni wagonjwa.

Spika wa Seneti Kenneth Lusaka amesema kuwa vikao hivyo vilisitishwa kwa kuzingatia agizo la Rais Uhuru Kenyatta la kukomesha safari za kuingia na kutoka jijini Nairobi ifikapo saa moja usiku kwa siku 21 zijazo. Hata hivyo shughuli jijini Nairobi zinaendelea kama kawaida isipokuwa tu kuanzia mwendo wa saa moja usiku.

Baadhi ya wajumbe walitangamana na watu waliopatikana na virusi vya corona

Taarifa zinaeleza kuwa hatua hiyo ilitokana na ujio wa baadhi ya wajumbe kutoka kwenye mataifa yaliyokuwa yameshambuliwa na virusi hivyo.

Katika kikao cha seneti kilichopita, seneta Kipchumba Murkomen alidai kuwa baadhi ya wajumbe walikuwa wametangamana na watu waliodhaniwa kuwa na ugonjwa huo akiwemo naibu gavana wa Kilifi Gedion Saburi aliyepatikana na ugonjwa huo, lakini akapona baada ya matibabu.