Home | Terms & Conditions | Help

November 25, 2024, 7:35 am

NEWS: WABUNGE CHADEMA WAJITETEA SAUTI ZILIZOVUJA

Dar es Salaam. Wabunge wa Chadema, Saed Kubenea (Ubungo) na Anthony Komu (Moshi Vijijini) wamesema sauti zinazosambaa katika mitandao ya kijamii zikidaiwa ni zao wakizungumzia masuala ya uchaguzi wa chama hicho, ni za kutengeneza.

Wakizungumza na waandishi wa habari leo Jumamosi Novemba 23, 2019, Kubenea amesema sauti hizo zimehaririwa kitaalamu kuitaka Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) kuchunguza ili kubaini ukweli.

Katika sauti zinazodaiwa kufanana na zao, wamesikika wakizungumzia uchaguzi wa chama hicho na kupanga safu ya viongozi wenye nguvu ya kukivusha Chadema kuelekea uchaguzi mkuu wa 2020.

“Tunaiomba TCRA ifuatilie kuwabaini wahusika, binafsi nitawaandikia barua wachunguze kumbaini aliyeanza kuzisambaza sauti hizo mitandaoni,” amesema Kubenea.

Kubenea amesema waliozisambaza wana nia mbaya ya kutaka kuwagombanisha na mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe.

“Chama chetu ni cha demokrasia hivyo kuelekea kwenye chaguzi zetu tunatamani kuwe na ushindani lengo ni kupata watu makini watakao kiongoza chama kwenye harakati za kisiasa hasa kwenye uchaguzi ujao wa mwaka 2020,” amesema Kubenea.

Komu amesema kinachoendelea kwenye mitandao ni njama za kukiondoa Chadema kwenye reli kipindi hiki cha uchaguzi wake wa ndani.

“Hizi sauti zimehaririwa kwa ufundi, ninawaomba wanachama na wananchi wazipuuze ni uongo ambao una kiashiria cha kutaka kukipaka matope chama chetu,” amesema Komu.