Home | Terms & Conditions | Help

November 26, 2024, 4:58 am

NEWS: VIZIWI NURU YA KILIMO YAWAFIKIA

DODOMA: CHAMA cha Maendeleo ya Kilimo kwa Viziwi Tanzania (CHAMAKIVITA) kimejipanga kutoa elimu kwa viziwi ili kuwawezesha kulima kilimo cha kisasa.

Kelvin Nyema ambaye ni kiongozi mtendaji wa chama hicho amesema kuwa chama hicho kimejipanga kutoa elimu kwa viziwi ambao ni wakulima kwa lengo la kuwaondolea changamoto wanazokumbana nazo.

Nyema amesema licha ya viziwi kujihusisha na kilimo lakini wamejikuta wakilima bila kuwa na tija kutokana na kutokuwa na ueledi wa kutosha juu ya nambo ya kilimo na kutokujua msimu halisi.

Amesema kutokana na changamoto mbalimbali za kimawasiliano viziwi wengi ambao wamekuwa hawajui namna bora ya kulima kilimo cha kisasa ikiwa ni pamoja na kutofahamu majira halisi ya kilimo.

“Tumelazimika kuanzisha chama cha maendeleo ya kilimo kwa viziwi Tanzania kwa lengo la kuwakwamua viziwi ambao wanajihusisha na kilimo,wakulima wengi ambao ni viziwi wanalima lakini kilimo chao bado ni duni.

“Kutokana na changamoto hizo kwa sasa tutatoa elimu kwa wakulima ambao ni viziwi kwa lengo la kuwafanya wakulima hao walime kilimo cha kisasa na kutumia pembejeo ambazo zinaendana na msimu wa kilimo.

“Kama viziwi watapatiwa elimu bora ya kilimo wataweza kulima kilimo bora na kuwaodolea dhana ya viziwi kuwa tegemezi,tunatazamia kuwa baadhi ya wakulima ambao ni viziwi wapatao 300 watapatiwa elimu na wao watakuwa mabalozi kwa wakulima wengine kwa kutoa elimu ya kilimo bora” amesema Nyema.