Home | Terms & Conditions | Help

November 25, 2024, 12:48 am

NEWS: VIONGOZI 6 WA SEREKALI ZA MITAA MBARONI WIZI WA BIL 1.6

Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa nchini Tanzania (TAKUKURU), Mkoa wa Ilala inawashikilia viongozi wapatao sita wa Chama cha Wafanyakazi wa Serikali za Mitaa Tanzania (TALGWU Saccos) kwa ubadhilifu wa Sh bilioni 1.6.

Akizungungumza na waandishi wa habari leo Januari 10, 2020 Kamanda wa Takukuru mkoa wa Ilalal Christopher Myava amesema viongozi hao wanashikiliwa baada ya kubainika kutoa fedha kwa madai ya kuwakopesha wanachama 91.

Amesema hata hivyo walibaini kutokuwapo kwa wanachama hao 91 na hivyo kusababisha upotevu wa fedha hizo.

“Tunafanya uchunguzi wa vyama vyote vya ushirika kwani tumebaini baadhi ya viongozi wamekuwa wakijinufaisha kwa kufanya ubadhirifu,” amesema Myava.

Amesema pia wanawashikilia watu watatu wa waliokuwa wakijifanya watumishi wa umma na uchunguzi dhidi ya makosa yao utakapokamilika hatua za kisheria zitachukuliwa.

Myava amesema katika kuhakikisha wanabaini mianya ya rushwa na kupata njia sahihi nya kuishauri Serikali, wamefanya uchambuzi wa mfumo wa matumizi fedha za ruzuku ya uendeshaji.

“Tumefanya uchambuzi wa mfumo wa uandikishaji wa vitambulisho vya taifa (NIDA)ili kubaini kama kunaweza kuwapo kwa mianya ya rushwa na kutoa ushauri kwa Serikali,” amesema Myava.

Amesema katika kipindi hicho cha miezi mitatu wamefanya ukaguzi na ufuatiliaji wa miradi yenye thamani ya Sh bilioni 13.5 inayotekelezwa na Serikali ukiwamo wa ujenzi wa machinjio ya Vingunguti.