Home | Terms & Conditions | Help

November 24, 2024, 12:21 pm

NEWS: UMOJA WA ULAYA WAPIGA MARUFUKU WAGENI KUINGIA ULAYA

Viongozi wa Umoja wa Ulaya wamekubaliana kuweka mara moja marufuku ya kusafiri kwa raia wa kigeni wanaoingia Ulaya kwa muda wa siku 30 ili kudhibiti kuenea kwa virusi vya corona.

Umoja huo pia umeanzisha usafiri wa haraka kwa ajili ya kusafirisha vifaa muhimu vya matibabu, chakula na bidhaa nyingine, ili kurahisisha usambazaji wake ndani ya nchi wanachama.

Wakati ambapo visa vya COVID-19 vikiwa vimeongezeka barani Ulaya hadi kufikia zaidi ya wagonjwa 60,000 na zaidi ya vifo 2,700 viongozi wa nchi hizo wamechukua hatua mbalimbali kama vile kuifunga mipaka yao. Uamuzi huo umefikiwa katika mkutano wao uliofanyika kwa njia ya video na kudumu kwa zaidi ya saa tatu na kuungana pamoja katika juhudi za kuvidhibiti virusi hivyo ambavyo vimesababisha hasara za kiuchumi.

Umuhimu wa kuungana

Rais wa Baraza la Ulaya, Charles Michel amesema viongozi hao wameelezea umuhimu wa kushirikiana kufanya kila linalowezakana kukabiliana na janga la virusi vya corona pamoja na athari zake.

Amesema nchi 27 wanachama wa Umoja wa Ulaya zimekubaliana kuweka vizuizi vya mpakani haraka iwezekanavyo katika sekta ya utalii na biashara nyingine zisizo muhimu. Amesema mpango huo hautowahusisha wakaazi wa muda mrefu wa Umoja wa Ulaya, wanadiplomasia pamoja na baadhi ya wafanyakazi wa afya na usafiri.

Rais wa Halmashauri Kuu ya Umoja wa Ulaya, Ursula von der Leyen amesema pendekezo lake la kuweka vikwazo vya kuingia kwenye nchi za umoja huo limepata uungwaji mkono mkubwa kutoka kwa nchi wanachama. Amesema sasa ni jukumu la nchi hizo kulitekeleza na kwamba wameahidi kufanya hivyo mara moja.