Home | Terms & Conditions | Help

November 27, 2024, 3:26 am

NEWS: UCHAGUZI WA NIGERIA WAHAIRISHWA

Tume ya uchaguzi nchini Nigeria imetangaza kuahirisha uchaguzi mkuu wa rais na wabunge kwa juma moja, hatua inayokuja ikiwa ni saa chache tu zilikuwa zimesalia kabla ya wananchi wa taifa hilo hawajapiga kura.

Zoezi la upigaji kura lilikuwa lianze majira ya saa nne asubuhi kwa saa za Nigeria katika vituo zaidi ya laki moja na elfu 20 huku nchi hiyo ikiweka rekodi ambapo jumla ya wagombea 73 wanawania kiti cha urais.

Rais Muhammadu Buhari anawania kuchaguliwa kwa muhula wa pili lakini anakabiliwa na upinzani mkali kutoka kwa kiongozi mkuu wa upinzani na makamu wa rais wa zamani, Atiku Abubakar.

Hata hivyo mwenyekiti wa tume ya uchaguzi, INEC, Mahmood Yakubu, akizungumza na wanahabari usiku wa kuamkia siku ya upigaji kura, amesema kwa ratiba ilivyo, isingewezekana tena kwa uchaguzi huo kufanyika kwa wakati.

Tume ya uchaguzi sasa inasema uchaguzi uliokuwa ufanyika Februari 16, sasa umesogezwa mbele hadi Februari 23.

INEC imeongeza kuwa uchaguzi wa wabunge kuwania viti 360 katika bunge la kitaifa na viti 109 katika bunge la seneti, nao utafanyika siku hiyo hiyo ya tarehe 23.

Yakubu kwenye taarifa yake ameongeza kuwa uchaguzi wa magavana na ule wa bunge la wawakilishi, wenyewe umesogezwa mbele na sasa utafanyika Machi 9 mwaka huu.

Tume ya uchaguzi inasema imefikia uamuzi wake baada ya kutafakari kwa kina kuhusu masuala ya usafirishaji wa vifaa na kufika kwa wakati kwenye vituo, changamoto ambayo tume hiyo inasema isingewezekana kuwa na uchaguzi huru, haki na wakuaminika.

Tayari wagombe wawili kutoka vyama vikuu vinavyopewa nafasi kwenye uchaguzi huu vimekashifu hatua ya tume ya uchaguzi kusogeza mbele uchaguzi huo.

Mwenyekiti wa tume ya uchaguzi ameongeza kuwa kusogezwa mbele kwa uchaguzi huu kutatoa nafasi kwa tume yake kushughulikia changamoto ambazo zimejitokeza ili kufanya uchaguzi huo uwe wa kuaminika zaidi.

“Huu ulikuwa ni uamuzi mgumu ambao tume tumelazimika kuuchukua lakini ni wa muhimu katika kuhakikisha tunafanya uchaguzi ulio huru na wenye kuaminika kwa kuzingatia misingi ya demokrasia”. Alisema Yakub.

Hatua kama hii iliwahi kuchukuliwa pia mwaka 2015, ambapo tume hiyo iliahirisha uchaguzi kwa majuma sita kwa kile ilichosema kwa wakati huo hali ya usalama iliyohusishwa na uasi wa kundi la kiislamu la Boko Haram, uamuzi ambao ulionekana kama njama za kutaka kumpa muda zaidi aliyekuwa rais wakati huo Goodluck Jonathan dhidi ya upinzani kutoka kwa Muhammadu Buhari.

Kuelekea uchaguzi huu chama tawala cha rais Buhari cha All Progressives, kilidai kuwa chama cha upinzani cha PDP kinaandaa mpango wa kutaka kuharibu uchaguzi huu kwa kuiba kura na kununua kadi za wapiga kura.

Katika kipindi cha wiki tatu zilizopita, kumeshuhudiwa ajali tatu za moto kwenye maghala ya tume ya uchaguzi ambapo mamia ya kadi za wapiga kura ambazo zilikuwa hazijachukuliwa ziliharibiwa ikiwemo mashine za kutambua wapiga kura.